Na Boniface Wambura
MSAFARA
wa watu 27 wa kikosi cha timu ya Taifa (Taifa Stars) kinaondoka kesho
(Julai 30 mwaka huu) saa 10 jioni kwa ndege ya Air Tanzania kwenda
Afrika Kusini ambapo kitapiga kambi ya siku mbili kabla ya kuingia
Maputo kuikabili Msumbiji (Mambas).
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itawasili saa 9
asubuhi kesho (Julai 30 mwaka huu) kwa ndege ya Fastjet, na baadaye
jioni kuunganisha safari ya Afrika Kusini.
Mechi
hiyo ya marudiano ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika dhidi ya
Msumbiji itachezwa Agosti 3 mwaka huu Uwanja wa Taifa uliopo Zimpeto nje
kidogo ya Jiji la Maputo.
Msafara
huo wa Taifa Stars kwenda Afrika Kusini unajumuisha wachezaji 19 na
waliobaki ni maofisa wa Benchi la Ufundi lililo chini ya Kocha Mkuu Mart
Nooij kutoka Uholanzi.
Wakati
kiungo Mwinyi Kazimoto ametua leo (Julai 29 mwaka huu) nchini kuungana
na wenzake, washambuliaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wao
wataungana na wenzao kesho (Julai 30 mwaka huu) jijini Johannesburg
wakitokea Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Wakati
huo huo, Serengeti Boys imewasili salama jana (Julai 28 mwaka huu)
jijini Johannesburg, Afrika Kusini kwa ajili ya mechi ya michuano ya
Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 dhidi Afrika Kusini
(Amajimbos).
Mechi
hiyo ya marudiano ya raundi ya pili itachezwa Jumamosi, Agosti 2 mwaka
huu kwenye Uwanja wa Dobsonville uliopo Soweto kuanzia saa 9 kamili
mchana kwa saa za Afrika Kusini.
Timu
hizo zilitoka suluhu katika mechi ya kwanza iliyofanyika Julai 18 mwaka
huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam. Serengeti Boys
inahitaji ushindi kwenye mechi hiyo au aina yoyote ya sare ya mabao ili
ifuzu kwa raundi ya tatu.
Chapisha Maoni