AZAM FC imeingia fainali ya michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 20 kwa nchi za Maziwa Makuu, maarufu kama Rollingston baada ya kuifunga mabao 2-0 EMIMA, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo, Azam FC iliyoitoa Simba SC katika Robo Fainali, itakutana na Twalipo katika fainali ya timu za Manispaa ya Temeke tupu kesho Chamazi.
EMIMA iliyoitoa Yanga SC katika hatua ya 16 Bora na Mwambao ya Bagamoyo mkoani Pwani katika Robo Fainali, leo ilimalizwa mapema tu kipindi cha kwanza na Azam FC.
Jamil Mchaulu ‘Balotelli’ ndiye aliyeifungisha virago timu hiyo ya Tabata kwa mabao yake dakika za 18 na 44 na kufikisha jumla ya mabao matatu katika mashindano haya.
Kocha Mkuu wa Azam FC, Mcameroon Joseph Marius Omog kama kawaida yake alikuwepo uwanjani kuangalia vipaji vya akademi na baada ya mechi akasema; “Nina furaha, huu ni msingi mzuri kwetu, vipaji na uwezo katika akademi, inafurahisha sana,”alisema Omog.
Mapema katika Nusu Fainali ya kwanza, Twalipo iliitoa Ashanti United ya Ilala kwa bao 1-0, Uwanja huo huo wa Azam Complex.
Dakika 90 za mchezo huo zilimalizika bila bao na ilibaki moja tu kutimia dakika 30 za nyongeza mchezo uhamie kwenye penalti kuamua mshindi, lakini Suleiman Bofu akamaliza kazi.
Mshambuliaji huyo hatari alimalizia shambulizi la kushitukiza kuipatia bao lililoipeleka fainali Twalipo.
EMIMA na Ashanti zitamenyana katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu pia kesho Chamazi.
BY AZAM NETWAORK
Chapisha Maoni