Kikosi cha cha wachezaji 20 wa Azam FC kimeondoka Dar es Salaam kwenda Kigali, Rwanda kushiriki Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame michuano inayoanza wikiendi hii mjini Kigali, Rwanda.
Azam FC imechukua nafasi ya Yanga SC iliyoenguliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa kushindwa kuthibitisha kupeleka kikosi cha kwanza pamoja na kocha Mkuu, Marcio Maximo kwa mujibu wa kanuni za mashindano.
Yanga SC ilitakiwa hadi juzi jioni kuwa imethibitisha na kutuma kikosi, lakini haikufanya hivyo na CECAFA ikawasiliana na TFF kuwaambia wapeleke timu nyingine iliyo tayari na zali likawaangukia Azam FC.
Yanga SC ilitaka kupeleka kikosi cha vijana kwenye nashindano hayo, jambo ambalo CECAFA waliwakatalia wakiwaambia hiyo si michuano ya watoto.
Kikosi cha Azam kilichoondoka chini ya kocha Joseph Marius Omog raia wa Cameroon ni makipa; Aishi Manula, Mwadini Ally, mabeki Waziri Salum, Gadiel Michael, Shomary Kapombe, Abdallah Kheri, Aggrey Morris, Said Mourad na David Mwantika.
Viungo Kipre Balou kutoka Ivory Coast, Salum Abubakar, Mudathir Yahya, Himid Mao, Khamis Mcha ‘Vialli’, Farid Mussa na Joseph Peterson wa Haiti, wakati washambuliaji ni Mrundi Didier Kavumbangu, Leonel Saint- Preux wa Haiti, Kipre Herman Tchetche wa Ivory Coast na John Bocco ‘Adebayor’.
Azam FC, mabingwa wa Tanzania Bara, sasa wanaingia Kundi A katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Kagame ya 40 pamoja na wenyeji, Rayon Sport, Coffee ya Ethiopia, Atlabara ya Sudan Kusini na KMKM ya Zanzibar.
Kundi B lina timu za APR ya Rwanda, KCC ya Uganda, Flambeau de L’Est ya Burundi, Gor Mahia ya Kenya na Telecom ya Djibouti wakati Kundi C linaongozwa na mabingwa watetezi, Vital’O ya Burundi, El Merreikh ya Sudan, Polisi ya Rwanda na Benadir ya Somalia.
Timu 14 zinatarajiwa kushiriki michuano hiyo kuanzia Agosti 8 hadi 24 mwaka huu- jumla ya mechi 34 zikichezwa katika viwanja vya Amahoro na Nyamirambo, Kigali.
Azam itacheza mechi ya kwanza kesho jioni dhidi ya wenyeji Rayon Sport Uwanja wa Amahoro, baada ya
KMKM ya Zanzibar na Atlabara ya Sudan Kusini kumenyana katika mechi ya ufunguzi mchana.
Azam FC itarudi tena dimbani, Agosti 10 kumenyana na jirani zao KMKM, kabla ya kucheza na Atlabara Agosti 12 na kukamilisha mechi za kundi lake, kwa kumenyana na Adamma ya Ethiopia Agosti 16.
Na Azam fc
Chapisha Maoni