Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limeongeza kwa siku kumi muda wa kumalizika usajili wa wachezaji
wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza
(FDL) kutokana na kuchelewa kwa link ya mfumo mpya wa usajili (system)
kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Kwa mujibu wa CAF, link hiyo
itakuwa tayari kwa matumizi ndani ya siku tatu zijazo kutokana sasa. Hivyo,
mameneja wa usajili wa timu hizo kwa sasa wanatakiwa kukamilisha nyaraka zote
zinazotakiwa ili link hiyo itakapokuwa tayari waweze kuingiza usajili wao mara
moja.
Kuanzia msimu wa 2014/2015
mfumo unaotumika kwa usajili kwa klabu hizo ni wa elektroniki badala ya ule wa
zamani wa kutumia fomu za kawaida. Mfumo huo wa kisasa ambao pia unatumiwa na
CAF unaondoa upungufu uliokuwepo katika mfumo wa zamani.
Kutokana na mabadiliko hayo,
usajili sasa utamalizika Agosti 27 mwaka huu badala ya leo (Agosti 17 mwaka
huu). Kipindi cha pingamizi ni kuanzia Agosti 28 mwaka huu hadi Septemba 3
mwaka huu.
Kamati ya Sheria na Hadhi za
Wachezaji itakutana kati ya Septemba 6 na 8 mwaka huu kwa ajili ya kupitia
pingamizi na kuthibitisha usajili.
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL)
inayoshirikisha timu 14 itaanza Septemba 20 mwaka huu wakati ratiba inatarajia
kutoka mwezi mmoja kabla ya kuanza ligi hiyo. Ligi Daraja la Kwanza inatarajia
kuanza wiki ya kwanza ya Oktoba.
Mwisho wa kuombewa Hati ya
Uhamisho ya Kimataifa (ITC) kwa wachezaji wanatoka nje ya Tanzania ni Septemba
6 mwaka huu.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU
TANZANIA (TFF)
Chapisha Maoni