Ads (728x90)

Inaendeshwa na Blogger.


TAARIFA KWA UMMA JUU
YA SUALA LA JUMA
NYOSO
By Mbfc_admin | October 2, 2015
 Leave a comment
Bodi ya klabu ya Mbeya City ilikutana tarehe
29.09.2015 kwa dharula kulijadili suala ambalo
hivi sasa linaendelea kujadiliwa katika Umma wa
wanamichezo nchini likimuhusisha mchezaji wa
timu yetu Juma Said maarufu kama “Nyoso”
baada ya mchezo kati ya timu yetu na Azam Fc
uliochezwa tarehe 27.9.2015 katika uwanja wa
chamazi.
Katika kikao hicho yafuatayo yaliamuliwa:
1. Klabu iliunda kikosi kazi kuliangalia suala zima
na kikosi kazi hicho kilipewa masaa 86 na
kilifanya kazi kwa adidu za rejea zifuatazo:
(a) Kupitia rejea za mchezo husika na kuangalia
Mazingira na Asili ya suala zima lililojitokeza.
(b) Kupata Maelezo ya awali ya mchezaji wetu
juu ya suala lenyewe.
(c) Kufanya uchambuzi wa kisayansi wa mzizi wa
suala analohusishwa mchezaji kwa kushirikisha
watalaam wa Ushauri Nasihi na Saikolojia kisha
kuishauri Bodi.
Wakati kazi hiyo ikiendelea, Klabu ilipokea nakala
ya barua ya adhabu ya mchezaji wetu Juma Said
maarufu kama “Nyoso” yenye Kumb:TPLB/
VPL/766/15 ya tarehe 30.09.2015.
Kwa Mukhtasari ifuatayo ni taarifa ya klabu
baada ya kikosi kazi hicho kuwasilisha taarifa
yake.
Klabu inapenda umma wa wanamichezo nchini
ukajua kuwa inasononeka sana na matukio yoyote
yenye kuupunguzia ladha mchezo wa mpira wa
miguu kunakofanywa na mdau yoyote wa mchezo
huo. Mara zote klabu imekuwa ikisisitiza na
kusimamia nidhamu ya wachezaji na viongozi
muda wote wanapotekeleza majukumu yao.
Katika mchezo wetu wa ligi kuu namba 32
uliochezwa katika uwanja wa Chamazi tarehe
27.09.2015 inadaiwa mchezaji wetu tajwa hapo
juu alifanya kitendo cha udhalilishaji dhidi ya
mchezaji wa Azam Fc John Bocco.
Tarehe 29.09.2015 kamati ya masaa 72
inayoisimamia shughuli za bodi ya ligi ilikutana
na kutoa uamuzi wa kumfungia mchezaji Juma
Saidi Nyoso kutocheza mpira wa miguu kwa
kipindi cha miaka miwili na faini ya shilingi milioni
mbili kwa kufuata kanuni namba 37(24) za ligi
kuu toleo la 2015(Kwa mujibu wa barua TPLB/
VPL/766/15 ya tarehe 30.09.2015).
Ufuatao ni uchambuzi wa adhabu iliyotolewa
1. (a) Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa
bodi ya ligi ( Masaa sabini mbili) pamoja na
mambo mengine inashughulikia kufanya maamuzi
kwa masuala yote ambayo maamuzi yake
hayakatiwi rufaa kama yalivyoainishwa katika
kanuni namba 74 ya ligi kuu. Kanuni iliyotumika
kutoa adhabu 37(24) si miongoni mwa kanuni
ambazo hazikatiwi rufaa ni kanuni inayopaswa
kutumika na kamati ya Maadili au Nidhamu
ambayo kulingana na aina ya kosa linahitaji
kuthibitishwa pasipo shaka na pande zote
zinazohusika.
(b) Hata kama kanuni waliyoitumia ingekuwa ni
sahihi lakini tafsiri ya kanuni hasa maneno AU,
NA hayakutumika ipasavyo kwa kuwa walikuwa
na uchaguzi wa adhabu lakini adhabu hizo
haziendi pamoja kama kamati ilivyo tafsiri.
Adhabu imeangalia upande mmoja wa hisia ,
hivyo kutoa adhabu kubwa bila kuangalia upande
wa mchezaji husika. Pia Kamati imeunganisha
adhabu zote kwa pamoja wakati kanuni inatoa
nafasi ya adhabu moja kwa wakati mmoja.
“37(24) Mchezaji yeyote atakayepatikana na hatia
ya kufanya makosa makubwa ya kimaadili au
kinidhamu, au ya kibaguzi au yakidhalilishaji au
yatakayotafsiriwa kuwa ni ukiukaji mkubwa wa
taratibu za mchezo na ubinaadamu atatozwa faini
kati ya shilingi milioni moja mpaka milioni tatu
au/na kusimamishwa kushiriki michezo mitatu
mpaka kumi ya klabu yake yoyote atakayoitumikia
katika Ligi Kuu na mashindano mengine rasmi ya
TFF mitatu mpaka kumi ya klabu yake yoyote
atakayoitumikia katika Ligi Kuu na mashindano
mengine rasmi ya TFF atakayoitumikia katika Ligi
Kuu na mashindano mengine rasmi ya TFF au
kufungiwa kipindi cha kati ya mwaka mmoja na
miwili.”
2. (a) Klabu inapata shaka juu ya maamuzi ya
kamati husika kutokana na kikao kilichotoa
maamuzi kiliongozwa na Mwenyekiti wa kamati
hii ni Ndugu Said Mohamed ambaye pia ni
Mwenyekiti wa AZam Fc. Sisi tuna amini kwamba
kwa kuwa yeye ni kiongozi wa Timu ya Azam
aliwajibika kujitoa kusikiliza shauri.Lakini
hakujitoa na aliendelea kuongoza kikao hicho
huku akijua kwamba yeye ni mjumbe mwenye
maslahi na upande mmoja (AZAM FC).
(b) Mchezaji anayetuhumiwa (Juma Said Nyoso)
hakupewa nafasi ya kusikilizwa na kamati kama
misingi ya utendaji haki inavyohitaji (Principle of
natural justice), Klabu inaona mchakato mzima
wa usikilizaji wa shauri hili umeingia dosari hivyo
maamuzi na adhabu iliyotolewa inakosa sifa
kisheria.
3 Mazingira ya tukio lenyewe:
(a) Klabu inatilia shaka ushahidi uliotumika na
kutafsiriwa na kamati kufanya uamuzi
uliotolewa,kuna uwezekano mkubwa kuwa kamati
iliangalia picha ya mnato(Still Picture)iliyosambaa
punde baada ya mchezo huo na kuzua mjadala
miongoni mwa jamii bila kuangalia mazingira
mengine ya tukio hilo.
(b) Katika kipande cha picha mwendo(Video)
kinachoonesha chanzo cha tukio hilo ni baada ya
mchezaji wa AZam Fc mwenye jezi namba 20
iliyoandikwa Mudathir kumfanyia madhambi
mchezaji wa Mbeya City mwenye jezi namba
10,hii ilikuwa faulo yake ya tatu kwa mchezaji
huyohuyo bila kuonywa na mwamuzi,Juma Said
Nyoso akiwa kiongozi wa wachezaji wa Mbeya
City alimfuata Mwamuzi wa mchezo huo
kumueleza kuwa Mudathir amekuwa akimchezea
sivyo mchezaji huyo bila kuonywa,ndipo John
Bocco alipofika eneo ambalo alikuwepo
Mwamuzi,Juma Said Nyoso na mchezaji
Mwingine wa Mbeya City Fc aliyevaa jezi namba
15 (Christian Sembuli),John Bocco alimpiga kibao
usoni Christian Sembuli(Jezi 15) mbele ya
muamuzi, wakati John Bocco akifanya hivyo
Mudathir(Jezi 20)alizunguka mgongoni kwa John
Bocco na kumvuta sehemu za siri(korodani) za
Juma Said Nyoso na akarudi upande wa kulia
kwa mwamuzi, wakati Mudathir (20) akifanya
hivyo John Bocco alimkanyaga na kumpiga teke
Juma Said Nyoso.
Klabu inaamini wanaopaswa kuathibiwa ni
wachezaji wa AZam Fc John Bocco na Mudathir
(20) waliotengeneza mazingira ya kuharibu
taswira ya mchezo wa mpira wa miguu mbele ya
macho ya watu waungwana.
Mapungufu ya Jumla ya adhabu iliyotolewa:
1. Kamati badala ya kutumia Kanuni ya 37.7(F)
ambayo haikatiwi Rufaa wakaitumia Kanuni ya
37(24) ambayo inakatiwa Rufaa.
2. Kamati hawakumpa nafasi ya kujitetea
mchezaji husika kwa mujibu wa kanuni ya
37(24).
3. Mwenyekiti wa kamati hii ni Ndugu Said
Mohamed ambaye ni Mwenyekiti wa AZam Fc
hakusitahili kuongoza wala kuwemo katika kikao
hicho kwa kuwa alikuwa na maslahi na timu ya
Azam Fc ambao ndio walio mlalamikia mchezaji
Juma Said Nyoso.
Umma wa wanamichezo ujifunze nini kutokana na
suala hili
1. Mamlaka zinazosimamia mchezo wa mpira wa
miguu ni vizuri sasa kutafsiri kwa upana dhana
ya “udhalilishaji” katika mpira wa miguu.
Hii inatokana na namna ambavyo suala hili
limeripotiwa na wadau mbalimbali wa mpira wa
miguu na wanaharakati,picha za tukio hilo
zilisambaa kila uchao.
Klabu inaamini kwa namna wadau walivyolijadili
na kulichambua suala hili,lilimdhalilisha zaidi
muhusika,kuwekwe utaratibu na chombo
ambacho kipewe jukumu la kupitia mashauri na
ushahidi wa matukio yanayotafsiriwa kuwa ni ya
“udhalilishaji” ili kuendelea kulinda heshima za
wahusika katika jamii.
Klabu imewasilisha Tff maelezo ya kutoridhishwa
na adhabu aliyopewa Juma Said Nyoso.
Imetolewa na
E.E.Kimbe
KATIBU MKUU
MCC FC
2/10/2015



Chapisha Maoni