BAADA ya kusota kwa muda mrefu katika ligi daraja la
kwanza timu ya soka ya Maji Maji Maarufu kama ‘wanalizombe’ toka mkoani Ruvuma
imefanikiwa kurudi ligi kuu baada ya kuifumua Mlale JKT bao 2-1 hivi karibuni katika mtanange wa ligi
daraja la kwanza uliofanyika kwenye uwanja wa Maji Maji Songea.
Maji Maji mabingwa wa kombe la Muungano mwaka
1985,1986 pamoja na 1998 imefanikiwa kurudi ligi kuu ya Vodacom toka iliposhuka
kwa mara ya mwisho msimu ya mwaka 2010/2011 baada ya kutokea mgogoro kati ya
wanachama pamoja na viongozi tatizo likiwa ni wasi wasi wa wanachama kuhusu
matumizi ya pesa za timu toka kwa mdhamini wao.
Akizungumza na Jelamba viwanjani Meneja wa timu hiyo God
Mvula alisema baada ya kupata ushindi dhidi ya Mlale JKT mji wa songea na
viunga vyake ulizizima kwa furaha na vifijo huku mashabiki wa timu hiyo
wakicheza ngoma ya Lizombe ambayo ni maarufu sana mkoani Ruvuma.
“tumepanda ligi kuu kulingana na msimamo wa ligi
ulivyo kilichobaki ni kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi yetu ya mwisho
dhidi ya Kimondo ili kuwadhiilishia wapenzi wa timu yetu kuwa tulijiandaa
vizuri na hatujabahatisha’alisema Mvula.
Pia Mvula alisema mara nyingi timu ya Maji maji
inashuka Daraja kwa tatizo la migogoro kati ya wanachama pamoja na viongozi suala ambalo wanalifanyia kazi kwa pamoja ili kuhakikisha
timu hiyo inaendeshwa kisasa na kurudisha makali yake ya zamani.
Timu ya maji maji imefikisha pointi 43 na kushika
nafasi ya pili nyuma African Sports ambayo imefikisha pointi 45 katika msimamo
wa kundi A ambapo kwa sasa kwa mtokeo ya uwanjani timu hizo zimepanda Daraja na
hakuna timu ambayo inaweza ikafikisha pointi hizo.
Chapisha Maoni