Kocha mkuu wa Yanga, Hans Pluijm
amesema wana ari ya kushinda mechi yao ya mwishoni mwa wiki hii dhidi ya
Etoile du Sahel licha ya kuwaacha wachezaji wake tegemezi katika
msafara wao wa Tunisia.
Yanga imeondoka Dar es Salaam Jumatano
usiku huku wachezaji wake tegemezi, wakiwemo Hassan Dilunga, Salum
Telela na Danny Mrwanda, aliyekuwa akicheza soka la kulipwa nchini
Vietnam wakiachwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kifamilia.“Yanga imesajili zaidi ya wachezaji 20, wote ni muhimu katika timu”.
“Ni kweli niliwahitaji katika mechi yetu ngumu dhidi ya Etoile, lakini sababu mbalimbali zimepelekea kuachwa kwao”, amesema Pluijm.
Yanga itacheza na wenyeji wao, Etoile du Sahel katika mechi ya marudiano ya raundi ya 16 bora ya michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika.
Katika mechi iliyochezwa wiki mbili zilizopita jijini Dar es Salaam, Yanga ililazimishwa sare ya 1-1 hivyo kuwa na kibarua kigumu cha kushinda ugenini huku wenyeji wao wakililia sare ili kucheza hatua inayofuata.
Chapisha Maoni