Klabu ya Daraja la Kwanza ya Sonderjyske
Fodbold ya nchini Denmark, imemnasa mshambuliaji Emmanuel Okwi na kumpa mkataba
wa miaka mitano.
Pamoja na dau la usajili kuonekana ni siri,
lakini Okwi atakuwa akilamba mshahara wa dola 10,000 (Sh milioni 20) kwa mwezi.
Kiasi hicho cha mshahara kinamfanya Okwi kuwa
mchezaji mwingine aliyeuzwa na Simba anayelipwa fedha nyingi nje ya nchi, baada
ya Mbwana Samatta ambaye TP Mazembe ya DR Congo inamlipa dola 10,000 kwa mwezi
pia.
Mkurugenzi wa Sonderjyske, Hans Jorgen Haysen,
ameiambia SALEHJEMBE, walikuwa wakimfuatilia Okwi kitambo sasa.
“Tulianza kumfuatilia baada ya kusikia taarifa
zake, wakati mwingine tuliambiwa na Kocha wa The Cranes (Uganda), Micho kuwa
ndiye Ronaldo wa Uganda. Tunafurahi kufikia naye makubaliano naye ya miaka
mitano na tayari tumesaini mkataba baada ya kuwa amefuzu vipimo,” alisema.
Kwa mujibu wa bosi huyo wa Sonderjyske, tayari
Okwi amepata kibali cha kufanya kazi nchini Denmark na jana alianza mazoezi
rasmi.
“Tayari ameanza mazoezi, tulifanya kazi ya
kumtambulisha na kumkabidhi jezi aliyokuwa akiitaka ambayo ni namba 25, baada
ya hapo amefanya mazoezi na wenzake.
“Kesho
(leo), tutacheza mechi ya kirafiki dhidi ya timu kutoka Ujerumani. Okwi atakuwa
kati ya watakaocheza ili kumtambulisha mbele ya mashabiki wa Sonderjyske,”
alisema Haysen.
Mshahara wa dola 10,000 unamfanya Okwi kupokea
mara tatu ya ule aliokuwa akilipwa Simba wa dola 3,000.
Ligi Kuu ya Denmark inatarajiwa kuanza wiki
ijayo na Okwi hatarejea Uganda, badala yake ataungana na wenzake kwa ajili ya
mazoezi na baadaye mechi za kirafiki halafu mechi za ligi.
Na Saleh Ally
Chapisha Maoni