HADI sasa, Mbwana Ally Samatta na
Mtanzania mwenzake anayecheza
naye TP Mazembe, Thomas
Ulimwengu wanajivunia rekodi mpya
waliyoweka, kuwa Watanzania wa
kwanza kucheza fainali ya Ligi ya
Mabingwa Afrika.
Na Samatta anajivunia pia rekodi ya
kuwa Mtanzania wa kwanza kufunga
bao katika Ligi ya Mabingwa Afrika-
baada ya kufunga bao la pili katika
ushindi wa 2-1 dhidi ya USM Alger
katika fainali ya kwanza Jumapili
iliyopita mjini Algiers.
Awali, Samatta na Ulimwengu
walivunja rekodi mbili zilizowekwa na
klabu ya Simba SC ya Dar es Salaam
mwaka 1974 na 1993.
1974 Simba SC iliweka rekodi ya kuwa
klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza
Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa
Afrika, walipotolewa na Mehalla El
Kubra ya Misri kwa penalti 3-0 baada
ya sare ya jumla ya 1-1, kufuatia kila
timu kushinda 1-0 nyumbani kwake.
Ni mechi ambayo Simba SC walirejea
na malalamiko kwamba kipa wao,
Athumani Mambosasa (sasa
marehemu) alifanyiwa fujo, wakati wa
upigwaji wa penalti ikiwemo kutishiwa
bastola.
Mwaka 1993 Simba SC iliweka rekodi
ya kuwa klabu ya kwanza ya
Tanzania kucheza fainali ya Kikombe
cha kwa Afrika kwa ujumla na Kombe
la CAF, ambalo sasa limekuwa Kombe
la Shirikisho baada ya kuunganishwa
na lililokuwa Kombe la Washindi.
Simba SC ilianza vizuri kwa
kulazimisha sare ya 0-0 mjini Abidjan,
Ivory Coast Novemba 12 dhidi ya
Stella kabla ya kufungwa 2-0 mjini
Dar es Salaam Novemba 26 mwaka
huo.
Samatta na Ulimwengu mwaka 2013
walivunja rekodi ya Simba SC kucheza
fainali ya Kombe la CAF walipoichezea
Mazembe katika fainali ya Kombe hilo,
wakifungwa 2-0 Novemba 23 na CS
Sfaxien nchini Tunisia kabla ya
kushinda 2-1 Novemba 30 mjini
Lubumbashi, Samatta akifunga bao la
pili dakika ya 24.
Na msimu huo, Samatta akawa
mfungaji bora baada ya kufungana
kwa mabao na raia wa Ivory Coast,
Vincent Die Foneye aliyekuwa
anachezea ENPPI ya Misri, kila mmoja
akifunga mabao sita.
Mwaka jana, 2014; Samatta na
Ulimwengu wakavunja rekodi ya
Simba SC kucheza Nusu Fainali ya
Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya
kuichezea Mazembe katika hatua hiyo
mechi ya kwanza wakifungwa 2-1
Septemba 20 na ES Setif nchini
Algeria na marudiano wakashinda 3-2
hivyo Setif kutwaa taji kwa faida ya
mabao ya ugenini baada ya sare ya
jumla ya 4-4.
Jumapili iliyopita Samatta na
Ulimwengu wakaandika rekodi mpya
ya kuwa Watanzania wa kwanza
kucheza Fainali ya Ligi ya Mabingwa,
huku Mbwana pia akiweka rekodi
binafsi ya kufunga bao katika mechi
hiyo Algiers.
Leo, Mazembe wakiikaribisha USM
Alger na mtaji wao wa ushindi wa 2-1
ugenini, Samatta na Ulimwengu
wanawania kuwa Watanzania wa
kwanza kutwaa Kombe la Ligi ya
Mabingwa Afrika.
Lakini pia Mbwana anawania kuwa
Mtanzania wa pili kuwa mfungaji bora
wa michuano hiyo, baada ya Mrisho
Ngassa aliyekuwa Yanga SC mwaka
jana, kabla ya kuhamia Free State
Stars ya mwaka huu.
Ngassa alikuwa mfungaji bora wa Ligi
ya Mabingwa Afrika msimu huu kwa
kufunga mabao sita akifungana na El
Hedi Belameiri wa Setif, Haythem
Jouini wa Esperance na Ndombe
Mubele aliyekuwa AS Vita ya DRC,
sasa Al Ahly.
Hadi sasa Samatta ana mabao sita,
akizidiwa moja na Sudan Bakri Al-
Madina wa El-Merreikh ya Sudan.
Samatta analingana na Mmorocco
Mouhcine Iajour wa Moghreb Tetouan
ya kwao, wakati Muivory Coast wa
Mazembe pia, Roger Assale ana
mabao matano.
Je, Mbwana Ally Samatta atavunja
rekodi ya Ngassa leo? Bila shaka hizo
ndizo dua za Watanzania kwa vijana
wao hao leo.
1. USM Alger wanacheza mchezo wa fainali
ya vilabu bingwa barani Afrika kwa mara ya
kwanza huku wakiwa bado wanamatumaini
ya kunyanyua ndoo hiyo kwa mara ya
kwanza katika historia ya klabu yao.
4. Idadi ya mataji ambayo TP Mazembe imewahi
kutwaa ubingwa wa vilabu barani Afrika.
Wametwaa ubingwa huo mwaka 1967, 1768,
2009 na mara ya mwisho kutwaa ubingwa huo
ilikuwa ni mwaka 2010.
5. Namba tano ni idadi ya wachezaji wa TP
Mazembe ambao walifanikiwa kutwaa taji hilo
kwa mara ya mwisho wakati klabu hiyo
ilipochukua ubingwa huo. Wachezaji hao ni
Robert Muteba Kidiaba, Joel Kimwaki, Jean
Kasusula, Given Singuluma, pamoja na Aime
Bakula ambao wanacheza fainali mwaka huu pia.
6.Idadi ya magoli ambayo yamefungwa na
mshambuliaji wa El Merreikh ‘El Medina’
Babeker, ambayo ni sawa na nyota wa TP
Mazembe Mbwana Samatta.
7. Ni idadi ya fainali za kombe la klabu bingwa
Afrika ambazo TP Mazembe imefanikiwa kucheza
katika historia ya klabu hiyo.
10. Idadi ya mataji ya klabu bingwa ambayo
vilabu vinavyocheza fainali nchi zao zimewahi
kutwaa kombe hilo, Algeria (5) na DR Congo (5).
13. Idadi ya mechi ambazo amecheza golikipa
wa USM Alger Mohamed Zemmamouche pamoja
na mlinzi wa TP Mazembe mwenye asili ya Mali
Salif Coulibaly. Wote wakiwa wamecheza kwa
muda wa dakika 1170 kila mmoja, hiyo
ikimaanisha wamecheza kuanzia mechi za 1/16
bora hadi hatua hii.
17. Jezi inayovaliwa na mchezaji wa TP
Mazembe Rainford Kalaba aliyefunga goli la
kwanza kwenye mchezo wa fainali ya kwanza
wakati TP Mazembe inaibuka na ushindi wa goli
2-1 dhidi ya USM lakini alitolewa nje kwa kadi
nyekundu kabla ya mapumziko na ataukosa
mchezo wa marudiano.
Kalaba amefuata nyayo za mzambia mwenzake
Given Singuluma ambaye alifunga goli mbili
kwenye mchezo wa fainali ya mwaka 2010
wakati TP Mazembe ikipata ushindi wa goli 5-0
dhidi ya Esperance kwenye mchezo wa kwanza
jijini Lubumbashi kabla ya kwenda kupata sare
ya bao 1-1 kwenye mchezo wa marudiano na
Mazembe kutwaa taji la Afrika kwa mara ya nne.
21. Idadi ya wachezaji wa kigeni
walioorodheshwa na TP Mazmbe kwa ajili ya
michuano ya klabu bingwa Afrika (Orange CAF
Champions League) kwa ajili ya mwaka 2015.
Mataifa hayo ni Cote d’Ivoire (wachezaji 3), Mali
(wachezaji 5), Malawi (mchezaji 1), Tanzania
(wachezaji 2), Zambia (wachezaji 4) na
Zimbabwe (mchezaji 1) wachezaji tisa pekee kati
ya 30 ndio wazawa wa Congo DR.
25. USM imefunga jumla ya magoli 25 kwenye
mechi 15 na kuwafanya wawe timu yenye magoli
mengi kwenye mashindano, magoli matano zaidi
ya wapinzani wao TP Mazembe.
39. Umri wa golikipa wa TP Mazembe Robert
Muteba Kidiaba na hiyo inamfanya aweke rekodi
ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa
kucheza fainali ya vilabu bingwa Afrika. Kidiaba
atakuwa akitarajia kutwaa taji hilo kwa mara ya
tatu akiwa na TP Mazembe baada ya kutwaa taji
hilo mwaka 2009 na 2010 lakini pia akiwa
amecheza dakika 1080 msimu huu.
76. Idadi ya magoli ambayo yamefungwa kwenye
dakika 15 za mwisho hiyo ni kati ya dakika 76
hadi dakika ya 90. Hiyo ni idadi kubwa ya magoli
yaliyofungwa kati ya dakika 15 za mwisho
kwenye idadi ya magoli yote yaliyofungwa hadi
sasa ambayo nimagoli 266.
Mgawanyiko wa dakika na magoli ni kama
ifuatavyo; dakika 0-15 (magoli 39), 16-30
(magoli 31), 31-45 (magoli 36), 46-60 (magoli
45) na 61-75 (magoli 39).
125. Idadi ya mechi ambazo zimeshachezwa
hadi sasa kwenye michuano hiyo na kushuhudia
jumla ya magoli 266 yakifungwa kutoka kwenye
michezo hiyo na kufanya wastani wa magoli 2.1
kwa kila mechi.
Chapisha Maoni