Ads (728x90)

Inaendeshwa na Blogger.



Michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) inayoshirikisha timu 24 zitakazocheza katika makundi manne ya timu sita sita kwa mtindo wa nyumbani na ugenini itaanza kutimua vumbi Novemba 22 mwaka huu.
Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyoketi jijini Dar es Salaam jana (Oktoba 29 mwaka huu) chini ya Mwenyekiti wake Geofrey Nyange ilipitia maandalizi maandalizi ya ligi hiyo ikiwemo mwongozo wake (roadmap).
Kwa mujibu wa mwongozo huo, usajili wa wachezaji utamalizika Oktoba 31 mwaka huu. Kipindi cha pingamizi ni kuanzia Novemba 1 hadi 7 mwaka huu wakati Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji inatarajia kukutana Novemba 11 mwaka huu kwa ajili ya kupitisha usajili.
Pia Kamati ya Mashindano imepitisha viwanja vya timu zote, isipokuwa uwanja wa timu ya Mpanda United ya Katavi na ule wa Town Small Boys ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Uwanja wa Town Small Boys haukupitishwa kwa vile hauna uzio wa kudumu ( wa chuma) wa kutenganisha wachezaji na washabiki, na pia ufikaji wa timu Tunduru ni mgumu kutokana na ubovu wa barabara ikizingatiwa kuwa ligi hiyo itachezwa hadi kipindi cha Masika.
Kwa upande wa uwanja wa Mpanda United, umekataliwa kwa vile hauna vigezo vya msingi vinavyotakiwa ikiwemo vyumba vya kubadilishia nguo, kutokuwa na nyasi na uzio wa kudumu kutenganisha wachezaji na washabiki.
Kutokana na uamuzi huo, Mpanda United sasa itatumia Uwanja wa Mandela uliopo Sumbawanga wakati Town Small Boys itachezea mechi zake kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.



Chapisha Maoni