TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Oktoba 5, 2014
STARS YAINGIA KAMBINI, WACHEZAJI WA NJE WATUA
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inaingia kambini kesho (Oktoba 6 mwaka huu) kujiwinda kwa mechi ya Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) dhidi ya Benin itakayochezwa Oktoba 12 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inaingia kambini kwenye hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam ikiwa na kikosi cha wachezaji 26 walioitwa na Kocha Mart Nooij kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 11 jioni.
Kwa mujibu wa Kocha Nooij, timu hiyo itakuwa na vipindi (sessions) 11 vya mazoezi kabla ya kucheza na Benin (Squirrels). Stars itafanya mazoezi asubuhi na jioni kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa ambapo baadhi yatafanyika Uwanja wa Taifa, na mengine kwenye uwanja mwingine.
Wachezaji Thomas Ulimwengu na Mbwana Samata wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) pamoja na Mwinyi Kazimoto anayechezea timu ya Al Markhiya ya Qatar wanawasili nchini kesho (Oktoba 6 mwaka huu).
Naye mshambuliaji Juma Liuzio anayechezea timu ya Zesco ya Zambia atawasili nchini keshokutwa (Oktoba 7 mwaka huu) kwa ndege ya Kenya Airways akitokea Ndola.
MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litakuwa na mkutano na waandishi wa habari kesho (Oktoba 6 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF, Jengo la PPF Tower.
MAFUNZO YA USAJILI LIGI DARAJA LA PILI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litaendesha mafunzo ya usajili kwa klabu za Ligi Daraja la Pili (SDL) yatakayofanyika kesho na keshokutwa (Oktoba 6 na 7 mwaka huu) kwenye hosteli ya TFF iliyopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume kuanzia saa 3 asubuhi.
Mafunzo hayo yatahusu usajili wa mtandao ambao ndiyo klabu hizo zitautumia kwa ajili ya Ligi hiyo itakayoanza baadaye mwezi ujao katika makundi manne ya timu sita sita kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.
Kesho mafunzo hayo yatakuwa kwa ajili ya maofisa wa usajili wa klabu za Abajalo, Arusha FC, Kiluvya United, Magereza Iringa, Milambo SC, Mji Mkuu (CDA), Mkamba Rangers, Mshikamano, Mvuvumwa FC, Navy, Njombe Mji, Singida United, Transit Camp, Volcano FC na Wenda FC.
Oktoba 7 mwaka huu mafunzo hayo yatahusisha maofisa usajili wa klabu za Bulyanhulu FC, Eleven Stars, JKT Rwamkoma, Kariakoo Lindi, Mbao FC, Mpanda United, Pamba, Town Small Boys na Ujenzi Rukwa.
MABADILIKO YA MECHI ZA FDL KUNDI B
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefanya mabadiliko kwa baadhi ya mechi za kundi B Ligi Daraja la Kwanza (FDL) baada ya kupokea barua kutoka Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) ikieleza kuwa Uwanja wa CCM Kirumba utatumika kwa shughuli za kidini kuanzia Oktoba 16 hadi 19 mwaka huu.
Kutokana na hali hiyo, mechi namba 17 kati ya Toto Africans na Green Warriors iliyokuwa ichezwe kwenye uwanja huo Oktoba 18 mwaka huu sasa itafanyika Oktoba 20 mwaka huu.
Mabadiliko hayo pia yameathiri mechi namba 19 kati ya Green Warriors na Oljoro JKT ambayo sasa itachezwa Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, Oktoba 23 mwaka huu badala ya Oktoba 21 mwaka huu.
Vilevile mechi namba 25 kati ya Burkina Faso na Oljoro JKT imesogezwa mbele kwa siku moja kutoka Oktoba 25 mwaka huu hadi Oktoba 26 mwaka huu. Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
BONIFACE WAMBURA
MKURUGENZI WA MASHINDANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
Chapisha Maoni