CHAMA cha Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC),
limeidhinisha pambano la ubingwa wa taifa uzani
wa kilo 69 litakalowakutanisha Ibrahim Maokola
dhidi ya Selemani Mkalakala.
Kwa mujibu wa Rais wa TPBC, Chaurembo Palasa,
pambano hilo limepangwa kufanyika Desemba 19,
mwaka huu kwenye Ukumbi wa Vigae Pub,
Mbagala jijini Dar es Salaam.
Palasa alisema pambano hilo litasindikizwa na
mapambano mengine ya utangulizi kati ya Abdallah
Mohamed dhidi ya Salehe Mkalekwa.
Alisema maandalizi kuelekea kwenye pambano hilo
ni mazuri na kwamba wanategemea mashabiki
wengi watajitokeza kuwaunga mkono vijana hao.
“Tumekuwa tukihamasisha mchezo wa ngumi
sehemu mbalimbali ili kuleta mvuto kwa wakazi wa
jiji na sehemu nyingine ili kuvutia wadhamini,”
alisema Palasa.
Alisema ngumi sio mchezo wa fujo kama baadhi ya
watu wanavyodhani, bali ni mchezo wa
wastaarabu ambao wanapigana kwa kufuata
sheria. Alisema atakayebainika kukiuka sheria
zilizowekwa awe ni bondia au promota
atachukuliwa hatua za kisheria.
Chapisha Maoni