CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinatarajia
kushiriki kwenye Mkutano Mkuu wa 78 wa Chama cha Kimataifa cha Waandishi
wa Habari za Michezo (AIPS) unaotarajiwa kuanza kesho (Jumatatu) Paris,
Ufaransa.
TASWA katika mkutano huo
itawakilishwa na Mwenyekiti wa chama, Juma Pinto na Katibu Mkuu, Amir Mhando
ambao wanatarajiwa kuondoka Dar es Salaam leo (Jumapili) alasiri kwa ndege ya
Emirates wakipitia Dubai.
Mkutano huo wa kawaida wa mwaka ambao utamalizika Machi 4, 2015
utashirikisha viongozi wa zaidi ya vyama vya waandishi wa habari za michezo 150
duniani, utaambatana na mijadala pamoja na semina mbalimbali kuhusiana na
uandishi wa habari za michezo.
Pia kutatolewa taarifa
kuhusiana na maandalizi ya michezo ya Olimpiki itakayofanyika mwaka 2016 Rio de Jainero, Brazil,
ambapo mhusika mkuu atakuwa Mkuu wa Masuala ya Habari wa Kamati ya Kimataifa ya
Olimpiki (IOC), Anthony Edgar.
Baadhi ya mada zingine katika
mkutano huo zitatolewa na wawakilishi kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa
(FIFA), Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA).Pia kutakuwa na uwasilishaji wa mada
kwa vyama mbalimbali vya kimataifa vya michezo.
Pia washiriki watapata
mafunzo ya changamoto zinazokabili uandishi wa habari za michezo kutokana na
kuenea haraka kwa mitandao ya kijamii.
TASWA
inalishukuru Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Kampuni ya Jambo Concepts
inayochapisha gazeti la JamboLeo kwa kugharamia tiketi za ujumbe huo.
TASWA ni
mwanachama hai wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Duniani (AIPS)
chenye makao yake makuu Lausanne, Uswisi, ndiyo sababu kila mwaka tumekuwa
tukishiriki mikutano hiyo.
Chapisha Maoni