Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), limetangaza viingilio vya mchezo kati ya timu ya Taifa ya Tanzania ya
Wanawake (Twiga Stars) dhidi ya timu ya Taifa ya Zambia (She-Polopolo)
kiingilio cha juu sh.5,000 kwa VIP na sh. 2,000 kwa majukwaa yaliobakia, mechi
hiyo itachezwa ijumaa jioni saa 10 kwenye dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar
es salaam.
Twiga Stars chini ya kocha
mkuu Rogasian Kaijage imeendelea kujifua katika hosteli za TFF zilizopo Karume,
kuhakikisha inaibuka na ushindi katika mchezo huo wa kuwnaia kufuzu kwa Michezo
ya Afrika nchini Congo- Brazzavile mwezi Septemba mwaka huu.
Katika mchezo wa awali
uliofanyika wiki tatu zilizopita jijini Lusaka nchini Zambia, Twiga Stars
iliibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya wenyeji Zambia, hivyo katika mchezo
wa ijumaa kuhitaji ushindi wa aina yoyote tu ili kuweza kufuzu kwa fainali
hizo.
TFF inawaomba wapenzi,
wadau na washabiki wa mpira wa miguu nchini, kujitokeza kwa wingi siku ya
ijumaa jioni uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kuja kuwapa sapoti Twiga
Stars watakapokuwa wanapeperusha bendera ya Taifa.
Wakati huo huo, timu ya
Taifa ya Wanawake ya Zambia (She-Polopolo) inatarajiwa kuwasili usiku wa saa
7.25 kuamkia alhmisi kwa shirika la Ndege la Ethiopia wakiwa na msafara wa
wachezaji 18 na viongozi saba na watafikia katika hoteli ya Tansoma iliyopo
eneo la Gerezani Kariakoo.
Msafara wa Zambia
(She-Polopolo) unaongozwa na mkuu wa msafara Lenny Khuwa, kocha mkuu Albert
Kachinga, kocha msaidizi Kape Saili, kocha wa magolikipa Yona Phiri, daktari wa
timu James Nyimbili, mchua misuli Conerlia Chazura, na meneja wa timu ni Besa
Chibwe.
Wachezaji wanaotarajiwa
kuwasili ni Rachel Nachula, Annie Kibanji, Chiko Nkhoma, Osala Kaleo, Joana
Benai, Meya Banda (Nahodha), Misozi CR Chisamu, Jane Nshika Chalwe, Milika
Limwanya, Mary Wilombe, Grace Chanda, Barbra Banda, Memory Mwaseba, Hazel
Natasha Nali, Martha Tembo, Mary Mwakapila na Ireen Lungu.
Kesho jioni She-Polopolo
wanatarajiwa kufanya mazoezi katika uwanja wa Taifa, uwanja ambao ndio utakaotumika
kw amchezo huo.
Waamuzi wa mchezo huo
kutoka nchini Uganda wanatarajiwa kuwasili leo mchana ambao ni Ms Anna
Akoyi , Ms Nakkito Nkumbi , Ms Jane Mutonyi, na Ms Nabikko Ssemambo,
Kamishina wa mchezo Ms Nomsa Jacobeth Mhalangu kutoka nchini Afrika
Kusini anatarajiwa kuwasili leo jioni.
Chapisha Maoni