MISS Tanzania mwaka 2000, Jacqueline Ntuyabaliwe ameacha historia ya aina yake nchini, baada ya kufunga ndoa na Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP, Dk. Reginald Abraham Mengi, tukio lililofanyika nchini Mauritius mwishoni mwa mwezi uliopita.
Jack, ambaye pia anafahamika kwa jina lake la kisanii kama K- Lynn, anaacha historia hiyo nchini Tanzania kwani licha ya kufunga ndoa hiyo akiwa tayari na watoto wawili mapacha aliozaa na mumewe, pia ndiye mshindi wa kwanza wa shindano hilo kubwa, kuolewa na bilionea baada ya kuwa katika uhusiano kwa miaka kadhaa pasipokuwa na kashfa na miezi minne baada ya kuvalishwa rasmi pete ya uchumba.
K-Lynn ambaye pia ni msanii wa muziki wa kizazi kipya, anaweka pia historia hiyo kwa kuolewa na mmoja wa wafanyabiashara wakubwa na wenye kuheshimika katika Afrika Mashariki, ambaye licha ya kumiliki vyombo vikubwa vya habari vikiwemo redio, magazeti na televisheni, pia ni mmiliki wa viwanda, migodi ya madini na biashara nyinginezo kubwa. IPP inamiliki vituo vya Radio One, Capital Radio, East Africa Radio, ITV, Eatv, Capital TV na magazeti la Nipashe, The Guardian na mengine kadhaa.
Harusi yao inayotajwa kuwa ni moja kati ya ndoa za kifahari nchini Tanzania, ilihudhuriwa na idadi ndogo ya watu wapatao 50, ambao ni ndugu wa karibu wa familia hizo mbili, pamoja na marafiki muhimu wa pande zote mbili.
Mengi, anayetajwa kuwa tajiri wa tatu nchini, miezi minne iliyopita, alimvalisha pete ya mchumba msanii huyo aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kufanya muziki, wakati wa sherehe ya kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa iliyofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa pia na watu wachache.
Baadhi ya washindi wengine wa shindano la Miss Tanzania walioolewa ni pamoja na Hoyce Temu (1999), Miriam Magese (2001) Faraja Kota (2004), Nancy Sumari (2005) na Sarah Israel (2011).
Chapisha Maoni