Kocha wa Real Madrid Carlo Ancelotti alikataa
kujibu maswali kuhusu hatima
yake baada ya mabingwa hao watetezi wa Ligi
ya Klabu Bingwa Ulaya kubanduliwa kwenye nusufainali na Juventus kwa
kulazwa kwa jumla ya mabao 3-2 Jumatano.
Mwitaliano huyo, aliyewahi kukufunza Juve, aliongoza Real kushinda
taji lao la 10 Ulaya msimu uliopita lakini anaelekea kumaliza msimu huu
bila taji lolote kubwa.
Hili haliwezi kukubalika katika klabu hiyo tajiri zaidi duniani,
ambako kumbukumbu huwa fupi na hakuna subira, na ambapo rais wao
Florentino Perez kwa kawaida hufuta makocha wakishindwa kushinda
vikombe.
Kikao cha Jumatano cha baada ya mechi kilitawaliwa na maswali kuhusu
hatima ya Ancelotti na iwapo atahudumu mkataba wake wote wa miaka
mitatu, ambao unamalizika mwisho wa msimu ujao.
“Hakuna maana sana kuongea kuhusu siku zijazo leo,” Ancelotti aliambia wanahabari.
“Kawaida ninaweza kujipa alama 10 kati ya 10 kwa sababu najitolea
sana kazini ingawa huwa sitaji kujipatia alama,” akaongeza mkufunzi huyo
mwenye umri wa miaka 55, ambaye alipoteza fursa ya kuwa kocha wa kwanza
kushinda Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mara nne.
"Tulifanya kila tulichohitajika kufanya. Tulishambulia sana. Tukapata
nafasi zetu. Ikiwa kuna jambo tunafaa kujilaumu kutokana nalo basi ni
mechi ya mkondo wa kwanza.”
Juve walitoka nyuma na kutoka sare 1-1 uwanjani Bernabeu kupitia bao
la fowadi wa zamani wa Real Alvaro Morata, baada ya kushinda mechi ya
mkondo wa kwanza mjini Turin 2-1.
Real wamo alama nne nyuma ya viongozi wa La Liga Barcelona zikiwa
zimesalia mechi mbili na walibanduliwa kutoka King's Cup na wapinzani
wao wa jiji Atletico Madrid Januari.
"Hatukucheza kwa ukali sawa kama tulivyofanya wakati huu ambapo tulijitolea kabisa,” Ancelotti alisema.
Real wanahitaji kujiinua upesi na kujiandaa kwa mechi yao ya La Liga
ugenini Espanyol Jumapili, siku ambayo Barca huenda wakatwaa taji lao la
tano la La Liga katika miaka saba wakishinda Atletico.
Kubanduliwa kwao Jumatano kutawauma zaidi Real na mashabiki wao kwani
Barca wamefuzu kwa fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya itakayochezewa
Berlin Juni 6 na fainali ya King's Cup dhidi ya Athletic Bilbao.
Klabu hiyo ya Catalona imo mbioni kurudia ushindi wa mataji matatu
makuu msimu mmoja sawa na ilivyofanya 2009, ilipoibuka timu ya kwanza,
na ya pekee, kutoka Uhispania kufanikiwa kufanya hilo.
Chapisha Maoni