Timu
ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imeendelea na mazoezi katika uwanja wa
Olympia Park kujiandaa na mchezo wa fungua dimba dhidi ya timu ya Taifa ya
Swaziland.
Kocha
mkuu wa timu ya Taifa Stars Mart Nooij amesema vijana wake wanaendelea vizuri
na mazoezi, ikiwa leo ni siku ya pili kufanya mazoezi baada ya kufanya mazoezi
ya kwanza jana jioni.
Nooii
amesema japokuwa kuna hali ya hewa ya baridi katika mji wa Rustenburg,
wachezaji wake wameanza kuizoea na kusema kwa kuwa bado kuna zaidi ya masaa 72
kabla ya mchezo wa awali watakua wameshaizoea hali ya hewa.
Kuhusu
uwanja wa mazoezi, kocha Nooij amesema hali ya uwanja ni nzuri, uwanja una
nyasi nzuri hali inayopelekea kikosi chake kufanya mazoezi katika mazingira
mazuri.
Akiongelea
mchezo wake wa kwanza wa ufunguzi dhidi ya timu ya Taifa ya Swaziland
utakaochezwa siku ya jumatatu, amesema anawajua Swaziland ni timu nzuri, mara
ya mwisho katika mchezo wa kirafiki walitoka nao sare, hivyo anawaanda vijana
wake kupata ushindi katika mchezo huo.
Kikosi
cha Swaziland kina wachezaji mchanganyiko wakiwemo wanaocheza ligi yao ya
nyumbani na baadhi wanaocheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini.
Taifa
Stars itacheza mchezo wa kwanza dhidi ya Swaziland katika Uwanja wa Olympia
Park siku ya jumatatu saa 1.30 usiku kwa saa za huku, sawa na saa 2.30 usiku
kwa saa za Afrika Mashariki.
Chapisha Maoni