Kocha Mkuu wa timu ya
taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Mart Nooij leo ametangaza kikosi cha wachezaji
28 watakaoingia kambini katika hoteli ya Tansoma iliyo eneo la Gerezani jijini
Dar es salaam, kujiandaa na michuano ya kombe la COSAFA na kuwania kufuzu kwa
AFCON na CHAN mwezi Juni mwaka huu.
Akizungumza na waandishi
wa habari leo makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), amesema wachezaji
28 aliowaita, amewaona kwa macho yake wakicheza, na katika wachezaji aliowaita
amechanganya wanaochipukia (damu changa) na wenye uzoefu wa michuano ya
kimataifa.
Nooij amesema katika
orodha hiyo ya wachezaji 28 watakaoripoti kambini jumatatu mchana, watapimwa
afya zao na madakatari wa timu ya Taifa, na kisha watakaokuwa fit atachagua
wachezaji 20 watakaokwenda kwenye michuano ya COSAFA nchini Afrika kusini.
Aidha Nooij ameongeza
wachezaji 8 watakaobakia nchini wanapaswa kuwa tayari wakati wowote wanaweza
jumuishwa katika kikosi kutokana na Taifa Stars kukabiliwa na michuano
mbalimbali ambayo pia inahitaji kuwa na wigo mpana wa wachezaji.
Wachezaji walioitwa na
kocha Nooij ni magolikipa: Deogratius Munish (Yanga), Aishi Manula, Mwadini Ali
(Azam), walinzi: Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Erasto Nyoni (Azam), Nadir
Haroub, Oscar Joshua, Kelvin Yondani (Yanga), Abdi Banda, Hassan Isihaka
(Simba), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar) na Haji Mwinyi (KMKM).
Wengine ni viungo: Amri
Kiemba, Salum Abubakar, Frank Domayo (Azam), Said Juma 'Makapu', Salum Telela,
Hassan Dilunga (Yanga), Said Ndemla (Simba), Haroun Chanongo (Stand United) na
Mwinyi Kazimoto (Al Markhiya).
Washambuliaji ni Ibrahim
Ajibu (Simba), Mrisho Ngasa, Simon Msuva (Yanga), John Bocco, Kelvin Friday
(Azam) na Juma Luizio (Zesco United).
Taifa Stars inatarajiwa
kuondoka nchini siku ya jumatano, Mei 13 saa 1 jioni kwa shirika la ndege la
Fastjet kuelekea nchini Afrika Kusini katika mji wa Rusterburg - North West
Province ambapo ndipo michuano ya COSAFA CUP itafanyika kuanzia Mei 17 mpaka
Mei 31 mwaka huu.
Mchezo wa kwanza wa Taifa
Stars iliyopo katika kundi B katika michuano ya COSAFA, itacheza dhidi ya
Swaziland Mei 18, Mei 20 (Madagascar Vs Tanzania) na Mei 22 ( Tanzania vs
Lesotho), mshindi wa kundi B atacheza robo fainali dhidi ya timu ya Taifa
kutoka Ghana.
Mara baada ya kumalizika
kwa michuano hiyo, Taifa Stars itarejea nchini kujiandaa na mchezo wa kuwania
kufuzu kwa AFCON 2017, dhidi ya Misri utakaopigwa Juni 13 nchini Misri, kisha
kurejea nchini kucheza na Uganda Juni 21 kuwania kufuzu kwa fainali za
wachezaji wa ndani CHAN.
Mart Nooij amesema
ataitumia michuano ya COSAFA kama sehemu ya maandalizi ya michezo ya kuwania
kufuzu kwa AFCON na CHAN.
IMETOLEWA NA MSEMAJI WA
TFF, BARAKA KIZUGUTO
Chapisha Maoni