ADEBAYOR AKIWA NA MAMA YAKE... |
ULIWAHI kusikia mshambuliaji Emmanuel Adebayor
amemfukuza mama yake mzazi kwenye jumba lake la kifahari?
Adebayor raia wa Togo na fowadi wa zamani wa Arsenal
amekuwa akikanusha hilo. Amekuwa akidai kuna matatizo lukuki ndani ya familia
yake.
Hivi karibuni alikwenda kuomba ushauri kwa
mshambuliaji wa Chelsea, Didier Drogba kuhusiana na suala hilo ambaye
alimshauri kuishi anavyoona ni sahihi si kuangalia watu wanataka nini.
Kama hiyo haitoshi, kupitia mtandao wa FaceBook,
Adebayor aliamua kuweka hadithi
nzima kuhusiana na matatizo yake kwenye mtandao wa Facebook
Jamaa amefunguka vilivyo na hii ndiyo barua
aliyotupia kwenye mtandao huo wa kijamii akieleza kila kitu kuhusiana na mama
yake, dada na kaka zake na kila kitu kilivyo.
Hakika inatia huzuni na kama kila kitu
alichoweka ni sahihi, huenda ikawa funzo kwa wanamichezo na wanasoka wa Tanzania.
Inachanganya ila anza kuisoma sasa.
“Niliamua
kuihifadhi hii stori kwa muda mrefu sana, lakini leo nimeamua kufunguka
kuhusiana na haya matatizo ya kifamilia ambayo yamekuwa yakinikabiri.
“Kweli
matatizo ya kifamilia hayawezi kutatuliwa hadharani hivi, lakini nimeamua
kufanya hivi huenda wengine wanaweza kujifunza kupitia kilichonitokea.
“Nikiwa
na umri wa miaka 17, ikiwa ni ajira yangu ya kwanza kama mwansoka, niliijengea
familia yangu nyumba nikitaka kuhakikisha wako.
“Unakumbuka
nilipotangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Afrika mwaka 2008, nilimpandisha mama
yangu kwenye steji ili kumshukuru. Mwaka huohuo nilimsafirisha hadi London kwa
ajili ya matibabu.
“Alipozaliwa
binti yangu, tulimpigia mama kumpa taarifa hiyo njema. Lakini ajabu alikata
simu haraka na hakutaka kusikia lolote kuhusiana na hilo! Unakumbuka, wakati
fulani watu waliwahi kushauri kwamba kutokana na matatizo yetu ya kifamilia
tungewasiliana na TB Joshua.
Mwaka
2013, nilimpa mama fedha, ili asafiri hadi Nigeria na kukutana na TB Joshua.
Alitakiwa kukaa wiki moja, lakini nilitaarifiwa kwamba aliondoka Nigeria baada
ya siku mbili tu! Achana na hilo, nilitoa fedha nyingi nikampa mama ili
aanzishe biashara ya biskuti.
“Pia
nikawaruhusu kutumia picha na jila langu ili waweze kuuza kwa wingi biskuti
hizo. Sasa nini hapo mtoto anaweza kufanya zaidi ya hapo ili kuisaidia familia
yake?
“Miaka
kadhaa iliyopita, nilinunua nyumba nchini Ghana, thamani yake ni dola milioni
1.2. Niliona kawaida kumuacha dada yangu aishi pale. Pia nilimruhusu Daniel
ambaye ni mdogo wangu kwa upande wa mzazi mmoja naye aishi pale.
“Miezi
michache baadaye, nilishangazwa baada ya kugundua dada yangu aliipangisha
nyumba ile na pia kumtimua Daniel! Nyumba hiyo yenye vyumba 15 sasa ilikuwa na
wapangaji, nilipompigia dada yangu kutaka kujua nini tatizo baada ya mimi
kwenda kwenye nyumba hiyo wakati wa kipindi cha likizo na kukuta lundo la
magari ya wapangaji, alinitukana kwa takribani nusu saa.
“Niliona
lingekuwa jambo zuri kuwasiliana na mama na kumuelezea hilo. ajabu naye
aliungana na dada yangu akitumia muda kama ule akiniporomoshea matusi na maneno
makali.
“Pamoja
na maneno ya kashfa nilionekana siisaidii familia. Lakini nikahoji hata gari
anayoendesha ni mimi ndiye nilimnunulia.
“Hiyo
ni kidogo, kaka yangu Kola Adebayor, sasa ameishi nchini Ujerumani kwa miaka
25. Anasafiri kurudi nyumbani kusalimia karibu mara nn kwa mwaka kwa gharama
amabzo nalipa mimi. Nalipa gharama zote za shule kwa watoto wake.
“Nakumbuka
aliwahi kuja hadi Monaco wakati nikiwa huko na kuniomba mtaji wa biashara.
Mungu ndiye anayejua kiasi cha fedha nilichompa. Leo biashara yenyewe iko wapi?
Lakini alipofariki kaka yangu Peter, huyu Kola akasema mimi ndiye ninahusika na
kifo chake! Kivipi?
“Kola
ndiye aliyekwenda katika gazeti la The Sun kuuza stori ili apate fedha. Kwa
pamoja, familia yangu walituma barua kwenye klabu yangu wakati nikiwa Real
Madrid kwamba nifukuzwe.
“Nikiwa
Monaco pia, nilipenda kuona familia yangu ina wanasoka wengine waliofanikiwa.
Nikajitahidi kuhakikisha mdogo wangu Rotimi anapata nafasi kwenye moja za
akademi bora za nchini Ufaransa.
“Unaweza
ukaona kama miujiza, kwani katika miezi michache tu, ndugu yangu huyo wa damu
alikuwa ameiba simu za wachezaji 21 kati ya 27 wa akademi aliyekuwepo!
“Siwezi
kusema chochote kuhusiana na kaka yangu Peter kwa sababu ameishatangulia mbele
ya haki. Lakini dada yangu Lucia Adebayor amekuwa akilazimisha nimlete Ulaya
kwa madai baba yangu alisisitiza nifanye hivyo. Nikimuuliza kwa nini,
anasisitiza kwa kuwa tu anataka kuja. Ulaya watu wako kwa sababu maalum!
“'Nilikuwa
Ghana, nikapata taarifa za ugonjwa wa Peter ambaye alikuwa taabani, nikaamua
kuendesha gari kwa kasi kubwa kwa lengo la kumuona na kusaidia pia.
“Nilipowasili
Togo mama akaniambia wala nisingekwenda, ningetuma fedha tu yeye
angeshughulikia kila kitu. Mungu ndiye anajua nilimpa kiasi gani cha fedha.
“Nilifanya
hivyo ili kumsaidia kaka yangu, leo watu wanasema sikufanya lolote kumsaidia
Peter. Kweli ningeweza kuendesha kwa masaa mawili tena kwa mwendo kasi kwenda
Togo?
“Mwaka
2005, nikaitisha mkutano wa familia ili tuweze kumaliza matatizo yetu.
Nilipowauliza kuhusiana na mawazo yao kuwa nini cha kufanya, wakashauri kuwa
niwanunulie ndugu wote nyumba ikiwa ni pamoja na kuwalipa mshahara!
“Leo
nikiwa hai, tayari wamegawana vitu vyangu utadhani niliishakufa. Imechukua kipindi
kirefu kwangu kufanikisha kusimama kwa foundation yangu. Hii ni kwa kuwa
wote hawakukubaliana na wazo langu la kusaidia watu wengine wakiona halikuwa
sahihi.
“Siandiki
hili kwa ajili ya kuwavua nguo wana familia kutoka katika familia yangu. Lengo
ni wengine wenye familia zao hasa kutoka Afrika wajifunze kupitia
yaliyonitokea.”
EMMANUEL ADEBAYOR
Chapisha Maoni