Ads (728x90)

Inaendeshwa na Blogger.




TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars chini ya Kocha wake Mkuu Charles Boniface Mkwasa imefanya mazoezi yake ya mwisho leo asubuhi katika viwanja vya hoteli ya Green Park Kartepe – Kocaeli nchini Uturuki.
Taifa Stars ambayo imeweka kambi nchini Uturuki kwa takribani wiki moja, inajiwinda na mchezo wake dhidi ya Nigeria siku ya Jumamosi Septemba 5, 2015 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa Afrika mwaka 2017.
Kocha Mkuu wa Stars Charles Mkwasa amesema anashukuru kambi imekua na mafanikio makubwa kwani vijana wanaonyesha mabadiliko makubwa sana.

                                                                                                       
Mkwasa amesema mazingira ya kambi yamekua mazuri, na katika mechi ya mazoezi dhidi ya Libya iliyochezwa siku ya ijumaa, vijana wake walicheza vizuri kwa nguvu na kufuata maelekezo yake, makosa machache yaliyojitokeza katika mchezo huo wameyafanyia kazi na sasa anaamini wako tayari kuwakabili Nigeria.
Mwisho Mkwasa amewaomba watanzania kujitokeza kwa wingi uwanja wa Taifa siku ya jumamosi  kuishangilia timu ya Taifa, kwani uwepo wa washabiki wengi uwanjani utawaongeza morali zaidi wachezaji na kujiona wapo nyumbani wanapambana kwa ajili ya Taifa lao.
Mara baada ya kuwasili Dar es salaam timu itaendelea na kambi kwa kufanya mazoezi mepesi siku ya jumatano pamoja wa wachezaji wa kimataifa Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Mrisho Ngasa katika uwanja wa Taifa kujiandaa na mchezo wa siku ya jumamosi dhidi ya Nigeria.

Wakati huo huo 

KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza kutotoza kiingilio chochote katika mchezo wa kuwania tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kati ya wenyeji Taifa Stars dhidi ya Nigeria (Super Eagles).
Taifa Stars ambao wameweka kambi nchini Uturuki wanatarajia kuikaribisha Super Eagles Jumamosi Septemba 5 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi zilizofanyika katika viwanja vya Zakhem Mbagala, Zitto, amesema kuwa mechi hiyo ni nyeti na Taifa Stars inahitaji kushinda ili kurejesha mazingira ya kufuzu mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).


Zitto alisema kuwa kutokana na Taifa Stars kupoteza mechi ya kwanza kwa kufungwa mabao 3-0 na Misri, timu hiyo inahitaji kushinda mchezo wake wa hapa nyumbani hapo Jumamosi.
Alisema kwamba hakuna timu inayokata tiketi ya kushiriki mashindano makubwa kama haijashinda mechi zake za nyumbani.




Chapisha Maoni