Ads (728x90)

Inaendeshwa na Blogger.




KAMA ilivyotarajiwa, Azam FC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Toto Africans Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam jioni ya leo.
Ushindi huo unaifanya timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake ifikishe pointi 25 baada ya kucheza mechi tisa, ikiwazidi kwa pointi mbili, mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 23. 
Katika mchezo huo, ambao wachezaji wa Toto waliingia na bango la kumuanga rasmi kocha wao, Mjerumani Martin Grelis, Azam FC walimaliza kipindi cha kwanza wakiwa wanaongoza 3-0.
Beki wa kulia Shomary Kapombe alifunga mabao mawili dakika za 34 na 36 mara zote akimalizia kazi nzuri ya winga Farid Mussa, wakati la tatu lilifungwa na Kipre Herman Tchetche dakika ya 45 akimalizia pasi ya kisigino ya Didier Kavumbangu.
Na mabao hayo yalikuja baada ya Toto kumpoteza kipa wake wa kwanza, Mussa Mohammed aliyeumia dakika ya 18 na nafasi yake kuchukuliwa na kipa wa pili, Said Omar. 
Azam FC nayo ilipata pigo dakika ya 33 baada ya kiungo wake wa ulinzi, Himid Mao kuumia pia na nafasi yake kuchukuliwa na Mnyarwanda, Jean Baptiste Mugiraneza.
Kipindi cha pili, Azam FC waliendelea kung’ara baada ya kupata mabao mawili, yaliyofungwa na Kavumbangu dakika ya 45 kwa shuti akimalizia pasi ya Ramadhani Singano ‘Messi’ na dakika ya 63 kwa shuti pia akimalizia pasi ya Mudathir Yahya.
Mchezo ulisimama kwa dakika zaidi ya 10 dakika ya 80 baada ya refa Anthony Kayombo kumruhusu kipa wa Azam FC Aishi Manula aende ‘kujisaidia’. Mugiraneza pia alitoka dakika ya 70 kwenda maliwatoni, ingawa yeye hakuathiri mchezo kusimama.
Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, JKT Ruvu wamepata ushindi wao wa kwanza msimu huu, baada ya kuilaza 2-0 African Sports Uwanja wa Mkwakwani, Tanga mabao ya Mussa Juma dakika ya 18 na Samuel Kamuntu dakika ya 90.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, David Mwantika, Aggrey Morris, Pascal Wawa, Himid Mao/Jean Mugiraneza dk33, Ramadhani Singano, Frank Domayo, Farid Mussa/Mudathir Yahya dk56, Didier Kavumbangu na Kipre Tchetche/Alan Wanga dk52. 
Toto Africans: Mussa Mohammed/Said Omar dk18, Erick Mlilo, Salum Chuku, Hamisi Suleiman, Hassan Khatib, Abdallah Seseme, Japhet Vedastus, Edward Christopher, Waziri Shentemba/Madinda Ramadhani dk59, Evarist Bernard na Miraji Athumani.
MATOKEO MECHI ZA LIGI KUU YA VODACOM TZ BARA
Leo; Novemba 1, 2015

Prisons 2-2 Ndanda FC
African Sports 0-2 JKT Ruvu
Azam FC 5-0 Toto Africans


MATOKEO-Mechi zilizopita:
Jumatano Oktoba 28
Toto African 1 Mgambo Shooting 0
Mwadui FC 2 Yanga 2
Mtibwa Sugar 1 Kagera Sugar 0
Mbeya City 1 Majimaji Fc 1
Ndanda FC 0 Stand United 0
Simba Sc 1 Coastal Union 0
Alhamisi Oktoba 2
Prisons 1 African Sports 0
JKT Ruvu 2 Azam FC 4
Jumamosi Oktoba 31
Simba 6 Majimaji FC 1
Kagera Sugar 0 Yanga 2
Mtibwa Sugar 4 Mwadui FC 1
Coastal Union 1 Mbeya City 1

Kesho; Novemba 2, 2015
Mgambo Shooting Vs Stand United







Chapisha Maoni