Ads (728x90)

Inaendeshwa na Blogger.


Ipo itikadi hata wengine huamini kwamba, utambulisho wa mtanzania ni alama ya chanjo ya mwili maarufu kama ‘ndui’  ambayo inapatikana kwenye bega mojawapo la mwilini mwa binadamu.

Lakini ukizungumza habari ya soka la Tanzania, lazima uguse uwepo wa vilabu viwili vya Simba na Yanga ambavyo vimetokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo ushirikiano wa vijana katika shughuli mbalimbali itikadi pia ikichangia kuanzishwa kwa timu hizi.

Yanga ndiyo kongwe kiumri ikiwa imeanzishwa rasmi mwaka 1935 Simba ikifuata mwaka mmoja baadaye 1936 ikiitwa Sunderland jina ambalo lilitokana na timu mojawapo ya ligi ya England wakati Yanga ilikuwa ikifahamika kwa jina la Young Africans SC ambalo ni chimbuko la jina la kimarekani. Baadaye viongozi wa serikali walivitaka vilabu hivi kubadilisha majina yao na kutumia majina halisi ya kiafrika na kuondoka kwenye majina ya kigeni, hapo ndipo tukapata Simba na Yanga.

Vilabu hivi vimejenga upinzani mkubwa katika soka la Tanzania tangu mwaka 1936 wakati huo ikichezwa ligi ya mkoa wa Dar es Salaam (Dar es Salaam League) hadi mwaka 1965 ilipoundwa ligi ya taifa lakini hadi leo vimekuwa vikiumiza vichwa vya mashabiki lukuki wa soka ndani na nje ya nchi kutaka kujua nani ataibuka na ushindi pale vidume hivi viwili vinapokutana.

Kwa mujibu ya mazungumzo ya wazee wa zamani, wanasema upinzani wao ulitokana na vyanzo vya kibaguzi. “Yanga na Simba sio kuna upinzani, kuna uadui. Uadui na upinzani wetu umeanzia pale timu ilipogawanyika kutokana na ubaguzi, kundi moja likiwa la waarabu jingine likiwa la wamatumbi, wandengereko na wazaramo”.

Matokeo yoyote ya timu hizi hugusa mashabiki kwa hisia tofauti, wengine huwa na shangwe kubwa wakati upande mwingine wakilia na kupoteza fahamu.

Oktoba 1 timu hizi zinakutana kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania bara, wanakutana kwa mara ya kwanza kwenye msimu wa 2016-2017 huku Simba wakiingia uwanjani wakiwa na machungu ya kupoteza michezo miwili mfululizo katika msimu uliopita wakikumbuka machungu ya September 26 mwaka uliopita sambamba na February 20 mwaka huu.

Takwimu zinaniambia timu hizi zimekutana mara 92 kwenye michezo ya ligi kuu Tanzania bara, Yanga ikiongoza kwa kushinda mechi 35 na ikiwa imefunga magoli 101 wakati Simba mechi 25 na kufunga magoli 88 huku sare zikiwa 32.

Mbali ya rekodi hiyo, tukiwatazama makocha wote wawili wamekuwa na historia ya tofauti. M-cameroon Joseph Omog ni kocha mpya wa Simba kwa sasa akiwa na michezo sita tu, ameshinda mechi 5 na kutoka sare mchezo mmoja. Kumbuka kocha huyu amerejea kwa mara ya pili, awali alikuja kuifundisha Azam FC ambapo aliipa ubingwa wa kwanza wa ligi.

Kocha wa Yanga Hans van der Pluijm raia wa Uholanzi yeye amesimama Yanga akiwa na rekodi lukuki ikiwemo kutwaa mataji matatu, mawili ya ligi na moja la FA lakini pia kuwafuta Yanga tongotongo za macho zilizodumu kwa miaka 18 tangu mwaka 1998 walipofuzu robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika hadi walipofuzu tena mwaka huu robo fainali ya kombe la shirikisho.

Katika rekodi nyingine, tangu Pluijm alipoifunga Simba February 20 mwaka huu, amecheza mechi 16 akishinda mechi 11 sare mechi nne na kupoteza mchezo mmoja wakati katika mechi 16 Simba ilishinda mechi 10 sare tatu na ikapoteza mechi tatu. Takwimu zinaendelea kuonesha, katika mechi hizo 16 Yanga imefunga magoli 34 Simba ikifunga magoli 22 wakati Yanga ikiruhusu wavu wake kuguswa mara 12 Simba imeruhusu wavu wake kuguswa mara 6 ikiwa ni nusu ya magoli waliyofungwa Yanga ndani ya mechi 16.

Mechi 7 za Yanga zilimalizika kwa ‘clean sheet’ yaani bila kuruhusu goli wakati Simba wakimaliza bila kuruhusu bao kwenye mechi 11. Ndani ya mechi 16, Yanga ilikusanya pointi 37 huku Simba ikitwaa pointi 33, Yanga ikapoteza pointi 11 huku Simba wakipoteza jumla ya pointi 15 katika michezo 16.

Kilichobaki ni macho na masikio ya wapenzi wa vilabu hivi kujua nini watafanya watani hawa wa jadi pale katika uwanja wa taifa chini ya usimamizi wa Martin Saanya. Je, Yanga wataendeleza ubabe au Simba watajibu mapigo katika msimu huu?



Chapisha Maoni