BAADA YA KUISHINDA YANGA, DK NDUMBARO AANIKA MATATIZO YALIYOKUWA KWENYE MKATABA WA OKWI
TAARIFA KWA UMMA
KUHUSU UAMUZI WA KIHISTORIA WA KAMATI YA SHERIA NA HADHI YA WACHEZAJI YA TFF
KATIKA SHAURI LA YANGA NA EMMANUEL OKWI
UTANGULIZI
Kwa
niaba ya mteja wetu, Emmanuel Arnold Okwi, napenda kutoa maelezo kuhusu Uamuzi
wa kihistoria katika soka la Tanzania ambao umefanywa na Kamati ya Sheria na
hadhi ya wachezaji ya TFF. Uamuzi huo ni wa kihistoria kwa misingi ifuatayo:
MOSI: Ni mara ya
Kwanza katika historia ya soka la Tanzania ambapo Kamati inakaa kujadili haki
ya mchezaji dhidi ya klabu kubwa na hatimaye kuamua kwa manufaa ya mchezaji,
tena pasipo kupiga kura kwa misingi ya upenzi na unazi. Kamati ya Mwanasheria
Mashuhuri na mwenye Msimamo Bw. Richard Sinamtwa iliamua kustafsiri kanuni kwa
kufuata ushahidi uliopo na kwa haki kabisa pasipo kujiingiza katika mtego wa
kupiga kura kama ambavyo tumekua tukiiona huko nyuma.
PILI: Kamati
ikiongozwa na Mwenyekiti ilitumia busara ya hali ya juu kwa kukataa ombi la Yanga
la kutengua uteuzi wa Bw. Hans Pope katika Kamati hiyo. Ikumbukwe kuwa Yanga
ilileta hoja ya kumkataa Bw. Hans Pope kwa misingi ya mgongano wa kimaslahi na
kumtaka mwenyekiti atoe uamuzi juu ya suala hilo. Endapo mwenyekiti angetoa
maamuzi ya kumuondoa Hans Pope, basi angejiingiza katika uvunjaji wa Katiba ya
TFF kwasababu yeye sio mamlaka ya uteuzi wa Hans Pope katika Kamati hiyo.
Mwenye mamlaka hayo ni Kamati ya Utendaji ya TFF. Hivyo Yanga walipaswa kuelewa
hilo na si kuishinikiza kamati, hususan Mwenyekiti, amuondoe Hans Pope kwenye
Kikao.
TATU: Maamuzi ya
Kamati yamefungua njia kwa wachezaji wengi ambao mikataba yao inachezewa na
vilabu kwa muda mrefu pasipo kuwa na nafuu yoyote ya kisheria kwa wachezaji hao
ambao ndio nguzo ya muhimu katika mpira wa Tanzania. Hata hivi sasa kuna
wachezaji ambao bado hawajalipwa stahili za mikataba yao ndani ya Yanga.
Tunawaomba wajitokeze ili tuwasaidie wapate haki zao za kisheria kama ambavyo
imetokea kwa Okwi.
NNE: Pamoja na madai
ya Yanga ya kukata rufaa FIFA / CAS, naomba wajue kuwa haki yao ya kukata rufaa
inatokana na ukweli kuwa Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya TFF
imetekeleza wajibu wake. Uamuzi huo wa Kamati umejenga msingi muhimu sana
katika suala zima la kuheshimu na kutekeleza mikakaba kwa mujibu wa kanuni za
FIFA. Endapo Yanga watakata rufaa kama wanavyodai, itakuwa ni hatua muhimu
katika kuhakikisha nguzo ya kuheshimu mikataba ya wachezaji inapewa msisitizo
unaostahili.
MGOGORO KATI YA
YANGA NA OKWI
Mkataba
wa Yanga na Okwi, ambao ulisainiwa tarehe 12 Disemba 2014 umekuwa na mapungufu
yafuatayo:
1.
Mkataba huo umempa majukumu mchezaji kufuatilia ITC na suala
zima la yeye kupata vibali vya kucheza. Hii ni kinyume na Kanuni za FIFA ambao
zinatamka bayana kuwa jukumu la kufuatilia ITC ni la wanachama wa FA, lakini
Yanga walimtwisha Okwi zigo hilo. Okwi alitekeleza jukumu hilo.
Kamati ililiona
hilo na kusema wazi kuwa hilo sio sahihi. Ni vema wachezaji wajue kuwa hilo sio
jukumu lao.
2.
Pili Yanga, kwa mujibu wa mkataba, walikuwa na haki ya
kumkata mchezaji theluthi moja ya mshahara wake wa mwezi endapo atakosa mechi
tatu au zaidi. Yanga walimkata Okwi Mishahara ya miezi mitano, kinyume na
matakwa ya mkataba na pasipo maelelzo yoyote.
3.
Yanga na Okwi walikubaliana kuwa mchezaji atalipwa ada ya
kusaini mkataba (signing on – fee) ya US$ 100,000, kwa Awamu mbili. Awamu ya
kwanza wakati wa kusaini mkataba na awamu ya pili tarehe 27 Januari 2014. Mpaka
hivi sasa, Yanga wamelipa US$ 50,000 tu na bado kuna deni la US$ 50,000. Huu ni
uvunjaji wa mkataba wa wazi kabisa.
4.
Kipindi chote mchezaji akiwa na klabu ya Yanga, hajapewa
nyumba kama ambayo walikubaliana. Huu ni ukiukwaji mwingine wa mkataba.
Baada ya Okwi kuanza kudai haki zake tajwa hapo juu, Yanga
waliamua kutomlipa mteja wetu mishahara ya miezi mitano kinyume na matakwa ya
mkataba kati yao.
MPANGO WA SIRI WA
YANGA
Yanga walikuwa na mpango wa siri wa kuvunja mkataba na
Emmanuel Okwi ili wamkomoe mteja wetu, ashindwe kucheza mpira, kiwango chake
kiporomoke na itumike kama onyo kwa wachezaji wengine ambao wanadai haki zao.
Mpango huu ulitekelezw kama ifuatavyo:
a.
Tarehe 27 Juni 2014, Yanga waliandika barua kwenda TFF, ikiitaka
TFF, pamoja mambo mengine, itambue kuwa mkataba kati yao na Okwi umefutwa.
Barua hiyo haikuwa na nakala kwa Okwi, ambaye ndiye upande wa pili wa mkataba
ambao unapaswa kufutwa.
b.
Tarehe 25 Julai 2014, Yanga waliandika barua ya pili
kukumbushia barua yao ya tarehe 27 Juni 2014. Barua hiyo ya pili haikuwa na
nakala kwa Okwi, ambaye ndiye upande wa pili wa mkataba ambao unapaswa kufutwa.
c.
Tarehe 20 Agosti 2014 Yanga waliandika barua nyingine tena
wakikumbushia hoja zao tajwa hapo juu. Kwa mara ya tatu, barua hiyo haikuwa na
nakala kwa Okwi, ambaye ndiye upande wa pili wa mkataba ambao unapaswa kufutwa.
d.
Yanga waliandika barua nyingine ya nne tarehe 25 Agosti 2014
ikiwa na hoja zile zile za kusitisha mkataba na mteja wetu. Kwa mara ya nne
barua hiyo haikuwa na nakala kwa Okwi, ambaye ndiye upande wa pili wa mkataba
ambao unapaswa kufutwa.
Baada ya TFF kupanga tarehe ya kikao cha Kamati ya Sheria na
hadhi ya wachezaji na kutoa barua ya wito tarehe 27 Agosti 2014 ndipo kwa mara
ya kwanza mchezaji Emmanuel Okwi akafahamu kuwa Yanga wameomba kuvunja mkataba
wake.
Tarehe 27 Agosti 2014, Emmanuel Okwi aliiandikia Yanga
KUKUBALI ombi lao la kuvunja mkataba.
Mambo muhimu ya
kujiuliza ni:
Mosi, Kama Mkataba ulikuwa
ni kati ya Yanga na Okwi, ni kitu gani kiliifanya Yanga ishindwe kumpa angalau
nakala ya barua nne ambazo ilizipeleka TFF?
Pili, Wakati Yanga
wanaomba kuvunja mkataba, walikuwa wameshamlipa Okwi stahili zake kwa mujibu wa
Mkataba huo?
Tatu, Je visingizio
vya kuvunjwa kwa mkataba wa Okwi vina uhusiano na idadi ya majina ya wachezaji
wa kigeni wa Yanga?
Ni bayana kuwa Yanga walitafuta kila aina ya kisingizio ili
mteja wetu aonekane kuwa ndio amevunja mkataba wakati ni wazi kuwa Yanga ndio
waliokuwa wa kwanza kuvunja mkataba huo tarehe 27 Januari 2014 kwa kushindwa
kumlipa mteja wetu US$ 50,000 za ada ya kusaini mkataba.
HOJA MBELE YA
KAMATI
Mbele ya Kamati Yanga walileta hoja kuwa: Hans Pope ana mgongano
wa maslahi kwa kuwa amemsajili Okwi Simba na yeye ni mjumbe wa Kamati hii; Okwi
amekataa kuongeza au kupunguza mkataba kama ilivyopendekezwa na Yanga; Okwi
ameleta madai yasiyo na msingi ya kutaka apewe nyumba ya kuishi; hajacheza
mechi 6 hivyo kuikosesha Yanga ubingwa. Okwi amefanya makubaliano na Klabu ya
Wadi Geldi ya Misri wakati ana mkataba na Yanga. Hivyo basi Yanga waliitaka
Kamati itamke kuwa mkataba kati yao na Okwi umesitishwa, imfungie Okwi kucheza
mpira Tanzania Maisha na ailipe Yanga dola za kimarekani laki mbili.
Tukimwakilisha Okwi, tulitoa hoja kuwa: Mteja wetu amekubali
ombi la Yanga la kuvunja mkataba ambalo limo katika barua zake nne; Yanga ndio
wamevunja mkataba kwa kushindwa kulipa signing fee US$ 50,000; Mishahara ya
miezi mitano US$ 15,000 na kodi ya nyumba US$ 2,800. Madai hayo ni kwa mujibu
wa mkataba.
Baada ya Maswali toka kwa Kamati kwa pande zote mbili, Yanga
waliomba kufuta barua zao, ombi ambalo lilitupiliwa mbali na kamati.
Kamati, hatimaye ilifanya maamuzi ya kihistoria katika
kulinda haki za kimkataba za wachezaji kama ambayo imeelezwa hapo juu. Kwa mtu
yoyote mwenye akili timamu, anapaswa kuipongeza kwa dhati kamati kwa maamuzi
ambayo wanajenga mpira wa nchi hii. Vilabu vinapaswa kufahamu kuwa haki za
mchezaji lazima ziheshimiwe.
Hoja za Yanga kuwa hakukuwa na madai ya fedha sio sahihi
kwasababu Majibu toka kwa Okwi na mabishano ya maneno mbele ya kamati hiyo
ilijadili kwa kina madai ya fedha ya Okwi na hata Yanga walikiri kutolipa madai
hayo. Hivyo basi si sahihi kusema kuwa eti suala la madai ya fedha halikujadiliwa.
(ona kiambatisho MNA1)
Msingi wa malalamiko ya Yanga ni barua ya tarehe 27 Juni
2014, ambayo hakuna sehemu ambayo inatamka suala la Simba. Kama kuna kesi dhidi
ya Simba, wasubiri wakati wa kupitia pingamizi za usajili lakini suala ambalo
Yanga walilalamikia ni kusitisha mkataba na Okwi na madai ya fidia.
Kamati ya Sheria na Mwenyekiti wake hawana mamlaka ya
kujadili uteuzi au uwepo wa Hans Pope kwenye kikao hicho. Mamlaka ya Uteuzi
ndio, kwa mujibu wa katiba ya TFF, yenye uwezo wa kutoa uamuzi kuhusu suala
hilo.
Kwa kuwa rufaa ni haki ya kila mtu, Uamuzi wa kukata rufaa
Fifa / CAS ni haki ya kisheria lakini tuwakumbushe Yanga kuwa “UKITAKA HAKI, TENDA HAKI KWANZA”.
DK DAMAS DANIEL
NDUMBARO (PhD)
Maleta &
Ndumbaro Advocates
Mawakili wa Mchezaji
Chapisha Maoni