Bayern Munich walithibitishwa kuwa mabingwa wa Ujerumani kwa mara ya 25 Jumapili baada ya Wolfsburg kulazwa 1-0 ugenini Borussia Moenchengladbach na kumaanisha kwamba sasa hawawezi kufikia klabu hiyo ya Pep Guardiola.
Straika Mjerumani anayechezea Gladbach Max Kruse alilituma taji hilo Munich kwa bao la ushindi la dakika ya 90 uwanjani Borussia Park lililopelekea Bayern kufunga wikendi wakiwa alama 15 mbele kileleni, na wakiwa na mechi nne walizosalia nazo.
Bayern walikuwa wametwaa ushindi wao wa 24 katika mechi 30 za ligi Jumamosi pale bao la dakika za mwisho la Bastian Schweinsteiger lilipowapa usindi wa 1-0 nyumbani dhidi ya Hertha Berlin uwanjani Allianz Arena.
Miamba hao wa Bavaria sasa wameshinda mataji matatu ya ligi ya Ujerumani mtawalia, huku Guardiola akishinda taji la Bundesliga kila msimu ambao wamewasimamia.
Mhispania huyo sasa ameshinda mataji 19 kama kocha, baada ya kushinda mataji 14 miaka minne aliyokuwa mdosi Barcelona, na tayari amenyakua vikombe vinne tangu kujiunga na Bayern Julai 2013.
Hakuna wakati, hata hivyo, kwa Bayern kusherehekea kwani wana mechi kali wiki chache zijazo wakiendelea kupigania marudio ya mwaka 2013 ya kushinda mataji matatu makuu – Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, ligi ya Bundesliga na Kombe la Ujerumani.
Watakaribisha nyumbani mahasimu wao wakuu Borussia Dortmund Jumanne nusufainali ya Kombe la Ujerumani, kupigania nafasi ya kufika fainali itakayochezewa uwanja wa Olimpiki jijini Berlin Mei 30.
Baada ya kushinda ligi, vijana hao wa Guardiola pia wanasubiriwa na nusufainali ya kukata na shoka Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya klabu aliyonoa awali Barcelona mechi ya mkondo wa kwanza ikiwa Mei 6, na mechi ya marudiano siku sita baadaye.
Chapisha Maoni