Msafara wa timu ya Taifa ya
Tanzania (taifa Stars) inayodhaminiwa na kampuni ya bia ya Kilimanjaro
Premium Lager tayari umewasili salama katika eneo la Borg El Arab jijini
Alexandria na kufikia katika hoteli ya Panacea tayari kwa mchezo wake
wa kesho.
Taifa Stars ambayo ilikuwa
kambini nchini Ethiopia kwa takribani wiki moja, iliondoka jana usiku
Addis Ababa na kuwasili uwanja wa ndege wa Cairo majira ya saa 8 usiku,
kisha kuunganisha kwa usafiri wa basi mpaka Borg El Arab takribani
masaa matatu.
Kocha mkuu wa Taifa Stars Mart
Nooij, atakiongoza kikosi chake katika mazoezi ya mwisho leo saa 1 usiku
katika uwanja wa Borg El Arab kwa saa za Misri, sawa na saa 2 usiku kwa
saa za Afrika Mashariki.
Akiongelea mchezo wa kesho, Nooij
amesema anashukuru kikosi kimefika salama nchini Misri na kipo katika
hali nzuri, vijana wana ari na morali ya hali ya juu, anaamini kesho
timu itfanya vizuri katika mchezo huo dhidi ya wenyeji Misri.
Nooij amesema mchezo wa kesho ni
muhimu kwake, na kikosi chake kitacheza mpira wa kasi na pasi za haraka
haraka, huku safu ya ushambuliaji ikihakikisha inatumia vizuri nafasi
itakazozipata.
Aidha kuelekea katika mchezo huo
wa kesho, kiungo Amri Kiemba ameungana na wachezaji wengine waliokuwa
kambini Addis Ababa kuchukua nafasi ya Mrisho Ngasa ambaye alishindwa
kuungana na timu kutokana na sababu zilizopo nje ya uwezo wake.
Naibu Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia tayari amewasili jijini Alexandria kwa
ajili ya kuipa sapoti Taifa Stars katika mchezo huo wa kesho.
Mchezo kati ya Misri na Tanzania
utachezwa kesho saa 2 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na kati katika
uwanja wa jeshi la Misri (Borg El Arab) uliopo takribani kilometa 70
kutoka jijini Alexandria na kilometa 200 kutoka jiji la Cairo.
Chapisha Maoni