Ads (728x90)

Inaendeshwa na Blogger.


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete
amesema kwamba siku hizi watu
wanapenda umaarufu wa vyeo vya
klabu na vyama vya michezo, lakini si
kufanya kazi ndiyo maana michezo
inadumaa nchini.
Akizungumza katika hafla maalum ya
kuagwa na wanamicheo, iliyoandaliwa
na Chama cha Waandishi wa Habari
za Michezo Tanzania (TASWA)
ukumbi wa Mlimani, City, Dar es
Salaam, Rais Kikwete alisema
anashangaa kwa nini michezo nchi hii
haiendelei.
Rais Kikwete alisema haoni sababu ya
michezo kutoendelea nchini wakati
kuna mazingira mazuri na katika
kipindi cha miaka 10 ya utawala wake
alijitolea mno kusaidia michezo.
Alisema kubwa alilofanya ni kusaidia
wataalamu kwa kuhakikisha kila
mchezo unapata kocha naye ndiye
anawalipa mishahara, lakini ajabu
baadhi ya vyama vya michezo
vilishindwa kundelea kufanya hivyo.
“Netiboli walianza vizuri, walikwenda
hadi Singapore kwenye mashindano
ya dunia, lakini baadaye
kilichowatokea sijui nini nini,”alisema.
Rais Dk. Jakaya akasema vyama
vinaweza hata kuajiri makocha
wazawa na wakaendelea kulipwa
kama walivyokuwa wanalipwa
makocha wa kigeni.
Akawageukia Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), ambao wameamua
kuachana na makocha wa kigeni na
kuajiri mzalendo, Charles Boniface
Mkwasa akiwaambia kwamba
wahakikishe wanamlipa kama
walivyokuwa wanalipa Wazungu.
Rais Kikwete amesema kwamba
msaada wake wa mwisho ambao
anawaachia wanamichezo wa
Tanzania, ni kituo cha kulea vipaji vya
wanamichezo wadogo cha Symbion
Power kilichopo eneo la Kidongo
Chekundu, Dar es Salaam ambacho
kitazinduliwa Oktoba 17, mwaka huu.
Amesema kituo hicho kilichojengwa
kwa msaada wa klabu ya Sunderland
ya England kina vifaa na viwanja vya
michezo aina yote, ukiwemo wa mpira
wa kikapu wa kiwango cha viwanja
vya Ligi ya Mpira wa Kikapu Marekani
(NBA).
Pamoja na hayo, Rais Kikwete
aliwashukuru TASWA kwa
kumuandalia shughuli hiyo na
akasema atamshauri mgombea Urais
kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe
Magufuli aendelee kuikumbatia
michezo.
Katika sherehe hizo za jana, Rais
Kikwete alikabidhiwa tuzo na TASWA
kumshukuru kwa mchango wake
mkubwa michezoni kwa kipindi cha
miaka 10 ya utawala wake.
Aidha, naye Rais huyo kipenzi cha
Watanzania alikabidhi tuzo kwa
Wanamichezo 10 waliofanya vizuri
wakati wa utawala wake. Rais pia
alikabidhi tuzo kwa viongozi
mbalimbali waliofanya vizuri pamoja
na wafanyabiashara na asasi
zilizomuunga mkono katika kupiga jeki
maendeelo ya michezo nchini.
Wanamichezo waliopata tuzo ni
Wanariadha Samson Ramadhan
aliyepata Medali ya Dhahabu mwaka
2006 katika Michezo ya Jumuiya ya
Madola, Martin Sule aliyepata Medali
ya Fedha katika Michezo ya Afrika
mwaka 2007 na Mary Naali aliyepata
Medali ya Shaba mwaka 2008.
Kikosi cha Taifa Stars kilichocheza
CHAN ya kwanza mwaka 2009 kilipata
tuzo, mchezaji Nitiboli Mwanaidi
Hassan, bondia Francis Cheka, kocha
Charles Boniface Mkwasa kwa
kuiwezesha timu ya wanawake, Twiga
Stars kucheza fainali za Afrika na
mshambuliaji Mbwana Samatta kwa
mafanikio yake TP Mazembe wote
walipokea tuzo.
Upande wa viongozi Jenerali Mstafu
Waitara kwa kujenga Uwanja wa Gofu,
Kanali Mstaafu Iddi Kipingu kwa
uwekezaji wake katika michezo ya
vijana, Dioniz Malinzi kwa kujenga
Uwanja wa Gofu Bukoba, Leodegar
Tenga kwa kuifanya TFF kuwa taasisi
yenye kuheshimika na Mtangazaji
Abdallah Majura kwa kuweza
kuanzisha kituo chake mwenyewe cha
Redio (ABM).
Makampuni na wadau waliopewa tuzo
ni pamoja na Bakhresa Limited kwa
mchango wao mkubwa michezoni na
TSN pia.
Rais Kikwete aliyeiongoza nchi tangu
mwaka 2005, anamaliza muda wake
mwishoni mwa mwezi huu na
anatarajiwa kukabidhi madaraka
baada ya uchaguzi Mkuu mapema
mwezi ujao.



Chapisha Maoni