Ads (728x90)

Inaendeshwa na Blogger.


AWALI ya yote niwape hongera wana Simba wote kwa uvumilivu mkubwa mlionao, hasa katika kipindi hiki kigumu ambacho mnapitia.
Kipindi kigumu kwa maana mbili kubwa. Kwanza najua wengi hamridhiki na nafasi tuliyopo hivi sasa kwenye msimamo wa ligi kuu inayoendelea nchini na pia wengi mmekuwa na sintofahamu kuhusu masuala mbalimbali yanayoendelea nje ya uwanja, hususan suala la kuvamiwa kwa eneo linalotarajiwa kujengwa uwanja linalomilikiwa na Klabu ya Simba kule Bunju jijini Dar es Salaam.
Naomba nianze na suala la wapenzi kutoridhika na maendeleo ya timu uwanjani, hususan kuwa kwenye nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kuu.
Siyo siri, Simba inapita katika kipindi kigumu sana, lakini kiukweli nafasi tuliyopo kimsimamo, siyo mbaya hata kidogo, ukilinganisha na klabu zilizopo juu yetu.
Tofauti yetu na timu inayoongoza Ligi Kuu Tanzania Bara ni pointi nne tu huku kila timu ikiwa imecheza michezo tisa.
Wapo wanaosema timu haichezi soka linaloburudisha, pia wapo wanaokwenda mbali zaid kwa kusema kwenye safu ya ushambuliaji kuna udhaifu mkubwa.
Kwa jicho langu, kuna eneo nakubaliana na baadhi ya mitazamo ya wakosoaji, ila niwaambie uongozi unazijua changamoto zote hizo, hususan kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji ambayo hata Kocha wa Simba, Dylan Kerr alitaka hivyo.
Taarifa njema kwa wana Simba ni kurejea kwa mchezaji wake Mkenya, Paul Kiongera, aliyekuwa kwa mkopo kwenye timu ya KCB ya nchini Kenya.
Lakini pia usajili wa Brian Majwega, mchezaji wa kimataifa wa Uganda aliyekuwa Azam FC, naye ataanza rasmi kuitumikia Simba mara ligi itakapoanza kwenye raundi ya kumi baadaye mwezi huu.
Mimi naamini kwa usajili huu, Simba itakuwa imepata suluhisho kwenye safu yake ya ushambuliaji, ukizingatia kupatikana kwa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ya mshambuliaji wetu, Danny Lyanga, sambamba na usajili wa beki mpya kutoka timu moja inayocheza ligi kuu nchini.
Naamini kwa usajili huo, ukichanganya na majembe yetu tuliyonayo, tutafanya vizuri msimu huu.
Tunachoahidi ni kuwapa matarajio yenu, tena kwa nguvu zote, la kuomba ni uhai tu.
La pili, nililopanga kuwaambia kwenye barua hii fupi, ni suala la uwanja wetu uliopo Bunju.
Zimeibuka porojo nyingi kuhusu uwanja wetu wa Bunju kuvamiwa na baadhi ya watu ambao wamejenga nyumba kwenye eneo hilo.
Binafsi nilipoziona hizi taarifa kwenye baadhi ya vyombo vya habari, nilishtuka sana, hata Rais wa Simba, Evans Aveva, naye alishtuka kupita kiasi na kuamua kuondoka mwenyewe kwenda kujionea kinachoendelea huko.
Kimsingi hakuna mtu au kikundi chochote ambacho kimevamia eneo hilo. Kilichoonekana kwa baadhi ya waandishi waliokwenda eneo hilo ni kuzionyesha nyumba zilizopo pembeni ya eneo la Simba na kusema kuwa zimejengwa ndani ya eneo letu, lakini siyo kweli.
Wakati mwingine najiuliza unawezaje kujua mipaka sahihi kama siyo kuwauliza wamiliki halali wa eneo husika au watu wa manispaa na wale wa ardhi?
Ni kuikosea heshima klabu kwa kiwango cha juu kuandika habari bila kufanya utafiti na kuwaweka wapenzi wetu roho juu bila sababu yoyote ya msingi.
Ninalowaomba wanachama na wapenzi wetu, wapuuze hizo taarifa, ni uongo mkubwa.
Matarajio yetu ni kuona habari za upotoshaji wa aina hiyo hazijirudii tena na sisi tutaendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vyote vya habari kwa kuzingatia misingi ya uandishi na utamaduni wa klabu.
Mwisho niishukuru timu ya Gazeti la Championi kwa kunipa fursa hii adimu ya kuongea na Wanasimba wenzangu kupitia safu hii.
Naamini Mhariri Kiongozi na rafiki yangu Saleh Ally, utanipa fursa tena na siyo kuongea na Wanasimba tu bali kutoa mchango wangu kwenye maendeleo ya mchezo huu murua zaidi duniani.



Chapisha Maoni