Taifa Stars na Malawi (Flames)
zinapambana Jumanne (Mei 27 mwaka huu) katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 11 jioni.
Mechi hiyo itakuwa ya mwisho kwa Taifa
Stars kujipima kabla ya kucheza mchezo wa marudiano wa michuano ya Afrika na
Zimbabwe (Mighty Warriors) utakaofanyika Juni Mosi mwaka huu jijini Harare.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro
Premium Lager ipo kambini Tukuyu mkoani Mbeya chini ya Kocha wake Mart Nooij
kujiandaa kwa mechi dhidi ya Malawi na ile ya Zimbabwe.
Malawi imewasili leo mchana (Mei 24 mwaka
huu) kwa ndege ya Malawian Airlines kwa ajili ya mchezo huo ikiwa na msafara wa
watu 27, na imefikia kwenye hoteli ya Sapphire Court iliyopo Mtaa wa Lindi
jijini Dar es Salaam.
Flames inayofundishwa na mchezaji wa
zamani wa kimataifa wa Malawi, Young Chidmozi inatarajia kufanya mazoezi leo
jioni Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Baada ya mechi hiyo, Malawi itakwenda
moja kwa moja nchini Chad kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika
itakayochezwa Mei 30 mwaka huu jijini Ndjamena.
Na Boniface Wambura, Dar es salaam
Chapisha Maoni