Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa
Stars) inatarajiwa kuingia kambini kesho jumatano katika hoteli ya
Tansoma iliyopo eneo la Gerezani jijini Dar es salaam kujiandaa na
mchezo dhidi ya Misri kuwania kufuzu kwa AFCON.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars Mart
Nooij, amewaita wachezaji 16 kuingia kambini kesho siku ya jumatano kwa
ajili ya kupimwa afya zao na kujua maandeleo yao kabla ya kuwajumisha
katika kikosi cha pamoja kitakachokua kwenye maandalizi ya mchezo dhidi
ya Misri.
Wachezaji walioitwa kuingia
kambini kesho ni, Mohamed Hussein, Peter Manyika, Hassan Isihaka, Jonas
Mkude (Simba SC), Salum Telela, Juma Abdul, Nadir Haroub (Yanga SC),
Aishi Manula, Mudathir Yahya, Frank Domayo, Kelvin Friday (Azam FC),
Rashid Mandawa, Atupele Green (Kagera Sugar), Haroun Chanongo (Stand
United) Malimi Busungu (Mgambo JKT) na Emmanuel Simwanda (African Lyon).
Mara baada ya kurejea kutoka
nchini Afrika Kusini, kocha wa Stars Nooij aliwapa mapumziko ya siku 10,
wachezaji waliokua kwenye michuano ya Cosafa mpaka Juni Mosi ambapo
ndipo watajumuika na wachezaji wengine waliopo kambini.
Ifikapo Juni Mosi, 2015 Taifa
Stars itaanza kambi ya moja kwa moja kujiandaa na mechi dhidi ya Misri
itakayochezwa jijini Alexandria katika uwanja wa Borg El Arab Juni 14,
2015 ikiwajumuisha pia wachezaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu
wanaocheza soka la kulipwa katika klabu ya TP Mazembe ya Congo DR.
Kabla ya kuelekea nchini Misri,
Taifa Stars inatarajiwa kuweka kambi jijini Addis Ababa nchini Ethiopia
kuanzia tarehe 4,Juni 2015 kwa muda wa wiki moja kabla ya kuelekea
nchini Misri kwenye mchezo huo dhidi ya Mafarao.
Juni 20, 2015 Taifa Stars
itawakaribisha Uganda kwenye uwanja wa Aman mjini Zanzibar katika mchezo
wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN,
zitakazofanyika nchini Rwanda 2016, na mchezo wa marudiano kufanyika
baada ya wiki mbili nchini Uganda.
Chapisha Maoni