Mechi ya Nani Mtani Jembe 2 kati ya
Simba na Yanga zinazodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itachezwa Jumamosi,
Disemba 13, 2014 saa kumi kamili jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es Salaam, Meneja Udhamini wa TBL, George Kavishe amesema kwamba
“Tayari Simba na Yanga zimesaini makubaliano ya kucheza mechi ya Nani Mtani
Jembe 2 (Nani Mtani Jembe 2 Match). Pambano hili ni zawadi ya kufungia mwaka
kwa mashabiki na kila timu imetia saini makubaliano kwamba itachezesha kikosi
cha kwanza ili kuwapa mashabiki burudani ya uhakika.”
Kavishe aliongeza kuwa mechi hii ni
maalumu kwa ajili ya kuhitimisha kampeni ya Nani Mtani Jembe 2 ambayo
imeendeshwa kwa zaidi ya miezi miwili ikiwapa fursa mashabiki wa timu hizi
kuchangia timu zao kila wanapoburudika na bia ya Kilimanjaro Premium Lager.
Alisema Nani Mtani Jembe 2 inahusisha
mashabiki wa klabu za Simba na Yanga ambapo zawadi ya shilingi milioni 100
itatolewa na kugawanywa ifuatavyo.
Shilingi Milioni 20 ni zawadi ya
mechi ya Nani Mtani Jembe ambapo timu itakayoshinda itapata sh milioni 15 na
timu itakayofungwa itapata shilingi milioni 5.
Kampeni hii inaendeshwa kwa njia ya
sms ambapo mashabiki wanapiga kura kwa njia ya sms na shilingi milioni 80
zimegawanywa kati ya timu hizo mbili ambapo kila timu ilianza na shillingi
milioni 40 kwenye benki maalumu mtandaoni.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium
Lager, Pamela Kikuli alisema mashabiki wa Simba na Yanga wanaweza kushiriki kwa
kununua bia ya Kilimanjaro Premium Lager yenye ujazo wa mililita 500 ambapo
mteja atabandua ganda la kizibo cha bia ya Kilimanjaro Premium Lager na kuona
namba maalumu. Ataandika jina la timu yake (SIMBA au YANGA) ikifuatiwa na namba
hiyo ya kwenye kizibo ambayo anatuma kwenda namba 15415 na kwa kufanya hivyo
anakuwa amepunguza pesa taslimu shilingi 10,000 kutoka timu pinzani na
kuichangia timu yake.
Kikuli pia alizikabidhi timu hizo
jezi maalumu itakayovaliwa mahususi kwa ajili ya mechi hiyo na kuwahimiza
mashabiki waendelee kuzipigia kura timu zao na kikubwa kuhakikisha wanafika
uwanja wa taifa na kujionea wenyewe pambano hilo ambalo lazima mshindi apatikane.
Mkurugenzi wa Mashindano wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura aliwakaribisha
mashabiki na kuwaomba wajitokeze kwa wingi kwani hivi sasa timu hizo ziko
kambini zikijiandaa na mtanage huo wa kukata na shoka unaotarajiwa kuwa na
msisimko mkubwa.
Alitaja viingilio vya mechi hiyo
kuwa ni shilingi 30,000 kwa VIP B, 20,000/= VIP C, 15,000/= kwa viti vya rangi
ya chungwa kiingilio kitakuwa ni sh 15,000 huku viti vya bluu na kijani tiketi
zikiuzwa kwa sh. 7,000/=.
Wambura alisema pambano hilo
litakalosimamiwa na TFF litaanza saa kumi kamili na litachezwa kwa dakika 90 tu
ambapo kama muda huo timu hizo hazitafungana basi mikwaju ya penati itapigwa
ili mshindi apatikane.
Taji la Nani Mtani Jembe
linashikiliwa na Simba ambao waliwafunga mahasimu wao 3-1 katika mechi
iliyochezwa Disemba 21, 2013.
Chapisha Maoni