Ads (728x90)

Inaendeshwa na Blogger.


Real Madrid waliweka hai matumaini yao ya kuwapiku viongozi wa La Liga Barcelona pale bao kali la James Rodriguez lilipowawezesha kushinda 3-0 nyumbani dhidi ya wanyonge Almeria Jumatano.
Barca, wanaosaka taji lao la tano la ligi ya Uhispania katika miaka saba, walikuwa wamelaza Getafe 6-0 uwanjani Nou Camp Jumanne na wamo alama mbili mbele ya mahasimu wao wa jadi zikiwa zimesalia mechi nne.
Mabingwa watetezi Atletico Madrid walisalia mbioni kumaliza wa tatu na kufuzu moja kwa moja kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya pale Fernando Torres alipotoka benchi na kufunga bao la kushangaza na kuwapa ushindi wa 1-0 Villarreal.
Torres alipokonya difenda mpira katikati mwa uwanja dakika 16 kabla ya mechi kumalizika, na kuchomoka hadi eneo la hatari na kisha kumchenga kipa Sergio Asenjo kabla ya kufunga.
Barca wana alama 84, nao Real alama 82 na Atletico 75, sita mbele ya Sevilla, walioshinda 3-1 nyumbani kwa limbukeni wa La Liga Eibar na kupanda juu ya Valencia hadi nambari nne.
Valencia wanaweza kurejea tena katika nambari nne, ambayo inawapa fursa ya kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, wakiponyoka kichapo mikononi mwa klabu iliyo katikati mwa jedwali Rayo Vallecano Alhamisi.
Almeria walikaza kamba hadi muda wa mfupi kabla ya mapumziko Bernabeu pale Rodriguez alipopata mpira nje tu ya eneo la hatari na kuutuma eneo kona ya juu ya goli.
Mabingwa hao wa Ulaya, waliohangaishwa na majeraha, waliongeza jingine muda mfupi baada ya kipindi cha pili kuanza Mauro Dos Santos alipojifunga baada ya kuwekewa presha na mfungaji mabao bora wa La Liga Cristiano Ronaldo.
Fowadi huyo wa Ureno alishindwa kuongeza idadi yake ya mabao na akasalia na jumla ya 39 msimu huu, moja juu ya nyota wa Barca Lionel Messi aliyefunga mawili Jumanne.
Mkabaji kamili Alvaro Arbeloa alifunga bao nadra na kufanya mambo 3-0 dakika tano kabla ya mechi kumalizika, lake la tatu katika mechi 167 alizochezea Real La Liga, alipombwaga kipa Ruben Martinez baada ya kupokea pasi kutoka kwa Javier Hernandez.
"Hatuna uhakika Barca watapoteza alama lakini tuna uhakika tunaweza kushinda mechi zote nne tulizosalia nazo,” kocha wa Real Carlo Ancelotti aliambia kikao cha wanahabari.


Chapisha Maoni