Mabingwa Barcelona wamekata rufaa dhidi ya kadi za manjano walizoonyeshwa Luis Suarez, Ivan Rakitic na Thomas Vermaelen mechi yao ya kwanza La Liga msimu huu, waliyoshinda 1-0 ugenini Athletic Bilbao Jumapili.
“Klabu hii inachukulia sababu zilizoelezwa kwenye ripoti ya refa kuwa zisizokubalika na kwa hivyo imewasilisha rufani kwa kamati ya dimba,” Barca walisema kwenye tovuti yao (www.fcbarcelona.es) Jumanne.
Kwa mujibu wa ripoti ya baada ya mechi iliyoandikwa na refa Carlos Del Cerro Grande, Suarez na Rakitic waliadhibiwa kwa kumshika mpinzani wakitumia mikono yao naye Vermaelen akalishwa kadi kwa kumtega mchezaji wa Bilbao.
Mechi ijayo ya Barca ni ya kwanza nyumbani katika ligi msimu huu dhidi ya Malaga Jumamosi.
Kocha Luis Enrique huenda akaweza kumchezesha Neymar aliyerudi mazoezini mapema kuliko ilivyotarajiwa Jumatatu.
Fowadi huyo wa Brazil amekuwa akitatizwa na matumbwitumbwi, na kukosesha Barca thuluthi moja ya hatari yao kwenye mashambulizi safu inayojumuisha pia nyota wa Amerika Kusini Suarez na Lionel Messi.
Watatu hao walifunga mabao 122 katika mashindano yote msimu uliopita na kusaidia Barca kutwaa mataji ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, La Liga na King's Cup
Chapisha Maoni